Sunday, August 18

Hakimu awataka mashahidi kutoa ushahidi kwa siku tatu mfululizo Kesi Aveva

0


By Pamela Chilongola

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka umetakiwa kuwaanda mashahidi wote waliobaki watakaotoa ushahidi kwa siku tatu mfululizo katika kesi inayowakabili vigogo watatu wa klabu ya Simba.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Rais wa Klabu hiyo, Evans Aveva, Makamu wa wake, Geofrey Nyange na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe.

Wakili wa Takukuru, Leonard Swai alidai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba alisema shauri hilo litakapokuja mahakamani hapo tunawahitaji mashahidi wote waliobaki kufika kwa ajili ya kutoa ushahidi.

“Upande wa mashtaka tunategemea mtatuletea mashahidi wote waliobaki ambao nataka watoe ushahidi kwa siku tatu mfululizo,” alisema Simba.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 13 mwaka huu itakapotajwa na kuanza kusikilizwa ushahidi Mei15, 16 na 17 mwaka huu.

Katika kesi hiyo HansPoppe anakabiliwa na mashtaka mawili ya kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uwongo yeye pamoja na wenzake.

Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashtaka mengine zaidi ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha hizo bila mamlaka ya Kamati ya Utendaji ya Simba, kujipatia fedha isivyo halali (Aveva) na utakayishaji fedha yanayowakabili wote, Aveva na Kaburu.

Katika maelezo ya awali, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Machi 12, 2016, Klabu ya Simba ililipwa jumla ya Dola za kimarekani 319, 212 na Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya nchini Tunisia.

Kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni ada ya uhamisho wa mchezaji Emmanuel Okwi kwenda Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya nchini Tunisia.

Share.

About Author

Leave A Reply