Sunday, August 18

GOZI LA NG'OMBE – TFF: Watanzania ni wakarimu

0


By Nicasius Agwanda

Tunaishi ili tushuhudie, tuone, tuamini au tusiamini lakini mwisho wa siku ni lazima tushuhudie yale yanayofanyika na tunaweza kuwa sehemu yake au tusiwe lakini tutashuhudia.

Katika uso wa nchi yetu Tanzania iliyowahi kuitwa kichwa cha mwendawazimu na huwezi kumlaumu aliyesema kwa sababu kwa wakati huo alishuhudia na mboni zake zikasababisha kauli ya alichoamini.

Ilipita miaka 39 kabla ya mabao ya Saimon Msuva, Erasto Nyoni na Aggrey Morris hayajatupeleka katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) mwaka huu. Miaka 39 ya majaribio, jasho, machozi na damu.

Kipindi kirefu cha maisha ya binadamu ambaye amekaribia kuwa wa makamo bila ya kuwa na furaha kwenye soka.

Ni kipindi kirefu kwelikweli kwa wenye kumbukumbu nzuri na waliokuwepo ni kipindi ambacho Rais wa kwanza Julius Nyerere alikuwepo madarakani.

Inawezekana tulikuwa na kundi la bahati zaidi katika kipindi chote hiki na kundi ambalo tuliamua kulipa ugumu wenyewe kutokana na hesabu zetu mbovu lakini wakati ulikuwa wetu, iliandikwa na ilibidi itimie.

Chini ya Walles Karia ndio tumeenda Afcom, imeandikwa na haitafutika. Chini ya Emmanuel Amunike na mbinu zake tusizoziamini ndipo tulipofuzu kwenda Afcon, haibadiliki.

Pamoja na furaha tuliyokuwa nayo, tayari si ndwele na yalishapita, yajayo ya kuganga sina hakika kama tumeyajenga au tunayasimamia ipasavyo.

Hili linakuja baada ya siku za karibuni kusikia kuwa maandalizi ya Afcon ya vijana chini ya umri wa miaka 17 yanahitaji michango kupitia vyombo vya habari na akaunti imetolewa kuchangisha.

Si vibaya kuchangisha lakini mbona ni wiki chache mpaka mashindano yaanze? Uwezo wetu wa maandalizi ni swali kubwa la msingi ambalo nawaza kuhusiana na kila nyanja tunayoifikiria.

Taifa Stars itakwenda Misri, itakwenda bila Wema Sepetu, Mheshimiwa Makonda wala Pierre Likwidi. Itakwenda peke yake na mashabiki watakaoweza kwenda. Huwezi kufikiria kamati ya ushindi huko. Ni ngumu na wala halitakiwi kuwa jambo la kufikiria kwa Sasa.

Kikubwa ni kuwa muda uliobaki kwenye kalenda inaonyesha kuwa ni siku pungufu ya sitini mpaka kufikia kesho. Hiki ni kipindi sio tu cha kumuuza Feitoto kwenda nje bali kipindi ambacho kitaleta tija kubwa kwa nchi na mabadiliko ya soka letu.

TFF haijawahi kuwa nyumba salama kwa soka letu, lakini kipindi hiki wametuokoa na mafuriko, sitaki kuwaza ni kwa namna gani bali ni maisha ndio yamekubali tukiwa chini yao. Nimeamua tu kuwakumbusha kuwa muda ni huu, maandalizi ni sasa.

Hamasa iliyopo kwa nchi ni jambo pekee ambalo wanatakiwa kuwa wamelipigia goti na kulifanyia ishara ya msalaba. Maisha kwao yatakuwa rahisi kama watafanya mambo sahihi, mambo ya kimpira. Huu ndo wakati wa kujisafisha na kuanza kuzifanyia kazi zile ahadi zilizopo kwenye ilani ya uchaguzi ya Wallace Karia.

Uzuri zaidi ni kuwa Rais anafuatilia, mamlaka zimetoa macho na zina furaha. Ukifanya jambo jema tu wanakupongeza, wanakukumbatia na kukupa hamasa ya kuendeleza yaliyokuwa mazuri. Watanzania pia wanaamini safari ndio imeanza, mazuri yaje.

Nimependa mtiririko kuanzia Twiga Stars, Serengeti Boys na wale ‘Under 18’ waliopo Misri na sasa Taifa Stars. Ukijenga msingi imara una uhakika wa nyumba ya mjukuu wako, maana ukiruhusu nyufa mwanao atakuta umepanga.

Tunajifunza kusahau, kwa sababu Taifa Stars imetutuma tufanye hivyo. Tunapotezea yaliyopita kwa sababu Serengeti Boys wakiwa Rwanda walituomba hivyo. Mafanikio yao yametuweka pamoja. Sasa TFF ni wakati wa kukumbuka jambo moja tu la msingi, ukiwatendea jema Watanzania, utaupenda ukarimu wao. Tuanzie hapa na tuache fitna zile.

Share.

About Author

Leave A Reply