Sunday, April 21

GOZI LA NG'OMBE: Klopp; Tazama ndani ya mboni za mashabiki

0


By Nicasius Agwanda

Liverpool ipo chini ya wamiliki ambayo ni kampuni ya John W Hnery inayofahamika kama Fenway Group. Hawa waliibuka na kujaribu kuleta uwekezaji wa kimarekani ambao wengi walishaanza kuuchukuia na kutaka kujaribu kuleta mabadiliko ya kihesabu kwenye jiji la Liverpool na uwanja maarufu wa Anfield.

Jambo la kwanza walilofanya lilikuwa kujaribu kuirejeshea thamani klabu ya Liverpool na kisha kuanza programu za usajili zilizokuwa zimejaa mahesabu makali.

Mahesabu ambayo yaliendana na takwimu za wachezaji kabla hawajasajiliwa na namna gani wanaweza kucheza pamoja.

Hii kazi aliifanya mfalme wa Liverpool, Sir Kenneth Mathieson Dalglish maarufu kama King Kenny Dalglish.

Hata hivyo mahesabu haya hayakuwa sawa, Downing hakuwa aliyetegemewa kumfanya, Andy Caroll kuwa bora, Henderson alikuwa mtoto na utaratibu wote ukaonekana kushindikana.

Katika kuendelea kutafuta namna ya kuishi huku wakibana matumizi akaletwa kijana ambaye alionekana anaweza kufanana na falsafa zao za “moneyball theory”.

Hii ni mbinu ya kusajili wachezaji wanaoonekana wa kawaida kwenye timu zingine na kuwapa thamani kisha unauza wale wenye thamani kubwa huku ukiwa una uhakika kuwa hawa waliokuja watakua na kukupa thamani unayohitaji.

Brendan Rodgers akawa mhanga wa utaratibu huu lakini kwa pongezi kubwa alikuwa karibu kutwaa ubingwa wa EPL kabla Steven Gerrard hajauchukua na kuukabidhi kwa Manchester Cty mwenyewe.

Maisha hayakuwa sawa tena kwa Rodgers na hakuna usajili aliofanya ulionekana kuwa na tija ama kwenda vile alivyotaka iwe.

Mkono wa kwaheri ukamfuata na akaletwa mwanaume mmoja aliyeipindua Bayern Munich na kuifanya Borussia Dortmund kuwa moja ya vigogo huko Ujerumani. Mwanaume huyu aliitwa Jurgen Klopp.

Tangu akiwa anatambulishwa tu ungeweza kugundua kuwa angeweza kuwa na ndoa yenye uhusiano mzuri na uaminifu na klabu ya Liverpool.

Kuanzia kujiita The Normal One na kuwa ametupa kijembe kwa Mourinho mpaka kuingia kwenye fainali ya Carabao na Europa, vilikuwa vielelezo tosha vya mtu ambaye Liverpool walikuwa wamemleta kwenye kuibadili timu.

Klopp kurejesha fulaa iliyopotea kwa kipindi cha miaka ishirini na nane katika muda wake wa misimu mitatu kamili akiwa na Liverpool.

Aliamini kuwa angeweza kuingia kwenye vitabu vya historia na kuwa moja ya wanaume wachache ambao wanaweza kupata sanamu kwenye jiji la Liverpool.

Siku zimekimbia na sasa Liverpool ina Mohamed Salah mahala pa Downing, inaye Mane alipowahi kuishi Joe Cole na nyumba inalindwa na silaha nzito za Vigril Van Djik pamoja Alisson Becker ambao wamesajiliwa kwa bei za washambuliaji.

Liverpool ina kikosi kilichokamilika kuliko wakati mwingine wowote kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita na pia wanaongoza ligi kuu ya nchini England tukiwa katika mzunguko wapili.

Hakuna klabu iliyowahi kushindwa kuutwaa uchampioni wa EPL baada ya kuongoza ligi mwezi Januari.

Bahati nzuri nyingine ni kuwa kwa sasa Liverpool haipo kwenye mashindano mengine ya ligi za ndani ya England kama FA na Carabao hivyo wachezaji wanaweza kuweka akili zao kwenye kitu kimoja tu muhimu, yaani EPL.

Mchezaji wa zamani wa Manchester United na mchambuzi wa sasa, Gary Neville alisema wakati msimu ukiwa mwanzo kuwa inawezekana Liverpool ikaacha hata kuwaza klabu bingwa barani Ulaya hili watimize kiu ya muda mrefu ambayo imekuwa ndio fimbo ya kuwachapia.

Fimbo ambayo maumivu yake washabiki wa Liverpool wameyazoea lakini hayakuisha kuwatoa machozi kwa miaka inayoelekea thelathini sasa.

Ndani ya mioyo ya mashabiki wa Liverpool ni kuwa hayatojitokeza makosa ya Benitez ya msimu wa mwaka 2009 walipopoteza kombe wakiwa wanaongoza ligi baada ya Christmas, makosa ambayo yalijirudia tena mwaka 2014 ambapo Gerrard anaishi na sura ya Demba Ba kwenye ubongo wake mpaka atakapoingia kaburini.

Mashabiki wanaona neema, washabiki wanajiandaa kushangilia, washabiki wana furaha iliyojificha kwenye uvungu wa mioyo yao wakisubiri muda ufike na maajabu ya Klopp yatokee. Hii itakuwa sherehe dunia nzima, washabiki hawa wana machozi ya furaha wameyahifadhi na ukitizama vyema unaona. Klopp awatendee haki tu, awape hiki wachostahiki na atakuwa “legend” kuliko hata alivyokuwa wakati akiwa Dortmund.

Share.

About Author

Leave A Reply