Tuesday, July 23

Esperance, Al Ahly ni vita ya kisasi

0


Cairo, Misri. Al Ahly ya Misri inaongoza kwa mabao 3-1 dhidi ya Esperance ya Tunisia wakati wanakwenda katika fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kesho Ijumaa.

Mechi ya kwanza iliyochezwa Alexandria wiki iliyopita iliingia doa baada ya kulazimika kutumika kwa VAR (video assistant referee) kuamua penalti za Ahly, ambazo zote zilifungwa na Walid Soliman.

Wachezaji na makocha wa Esperance walimshtumu mshambuliaji wa Ahly, Walid Azaro kujiangusha kwenye eneo la hatari mara mbili na kupewa penalti hizo.

Miamba hiyo ya Tunisia imemshutumu mwamuzi Mualgeria kwa kuwapendelea Wamisri hao tangu katika kikao cha awali cha kuamua jezi, pamoja na kucheleweshwa kufika uwanjani na kunyanyaswa na polisi.    

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limemfungia Azaro kucheza mechi mbili, lakini wamekataa kuifuta kadi ya njano iliyolalamikiwa na Esperance kwa wachezaji wake Chamseddine Dhaouadi na Franck Kom. 

Vituko hivyo ya fainali ya Ligi ya Mabingwa vilitokea wiki mmoja baada ya kushuhudia aibu ya mwaka katika soka la Afrika katika mechi mbili za nusu fainali za mashindano ya CAF.

Esperance ilifunga miamba ya Angola, Primeiro Agosto mabao 4-2 jijini Rades na kufuzu kwa fainali baada ya polisi 51 na mashabiki kupambana uwanjani huku 12 wakikamatwa.

Mashabiki walirusha mvua ya mawe, na polisi walipiga mabomu ya machozi na kusababisha uwanja wote kujaa moshi, na kufanya kipindi cha pili kuwa kigumu kwa wachezaji.

Kocha Mserbia wa Primeiro, Zoran Manojlovic alisema hali hiyo ilikuwa kama kutazama “movi ya kutisa “, lakini CAF haikuchukua hatua yoyote.

Siku moja baadaye, Al Masry ya Misri wachezaji wake waligoma na kuondoka uwanjani kupiga bao la AS Vita Club ya DR Congo katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika uliofanyika Kinshasa.

Walidai mfungaji wa bao hilo alikuwa ameotea, lakini picha iliyoonekana katika video uwanjani hapo ilithibisha kuwa mwamuzi Mshelisheli alikuwa sahihi kukubali bao hilo.

Masry walirejea mchezoni baada ya dakika tano, lakini baada ya mechi hiyo hakupewa adhabu yoyote.

Share.

About Author

Leave A Reply