Friday, March 22

Dk Kijaji aagiza mtumishi wa TRA kusimamishwa kazi

0


Dodoma. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji, leo Desemba 3, 2018, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kumsimamisha kazi mfanyakazi wake mmoja mkoani Dodoma aliyemtaja kwa jina la Daniel Kingu kusudi kupisha uchunguzi.

Kingu anatuhumiwa kumbughudhi mfanyabiashara mmoja Jijini  Dodoma.

Dk Kijaji, ametoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwenye mitaa ya Jiji la Dodoma baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mfanyabiashara mmoja kwamba, amekuwa akipokea simu za vitisho kutoka kwa mfanyakazi huyo akishirikiana na watu wengine na kumtaka ampelekee shilingi laki saba kwa ajili ya kulipia mashine ya kutolea stakabadhi za kielektroniki (EFD) la sivyo angefungiwa biashara yake.

“Mteja wetu awe salama, nitaendelea kufuatilia, lakini kuanzia muda huu Kingu aondoke ofisini, hatuwezi kuwavumilia watu wa jinsi hii hata kidogo kwa sababu kazi ya kuuza EFD machine si yake na anamwambia mteja aende ofisini kwake chumba namba fulani, anafanya haya mambo ndani ya ofisi ya Serikali, akitoka nje inakuwaje,”  alihoji Dk Kijaji.

Amesema hatasita kuchukua hatua hizo kwa wafanyakazi wengine wa TRA popote walipo nchini wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili.

Pia amewataka watendaji wa TRA nchini kote kufanyakazi zao kwa kuzingatia maadili ya kazi, kukadiria kodi kwa haki,  watumie lugha nzuri kwa wateja wao na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu wa wafanyabiashara katika masuala ya kodi badala ya kuwakadiria kodi kubwa isiyolipika.

“Ni lazima tuwalee wafanyabiashara hawa wadogo, ndiyo watakaotulipa kodi kubwa huko mbeleni badala ya kuwaumiza tangu wanapoanza biashara zao,” amesema naibu waziri huyo.

Naye Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Thomas Masese ameahidi kutekeleza maagizo hayo na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo huku naye akirejea wito kwa watumishi wa Mamlaka hiyo mkoani Dodoma kufanyakazi bila kuwanyanyasa wafanyabiashara na waepuke kujihusisha na vitendo visivyofaa kama vya kuomba rushwa.

Share.

About Author

Leave A Reply