Tuesday, March 19

Dk Bashiru amtaka Membe ajifunze hekima za Lowassa

0


Geita. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amemmiminia sifa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akisema kuwa ni mtu muungwana na hana unafiki na kumtaka Bernard Membe kuiga tabia hiyo.

Akizungumza jana usiku Desemba 2, 2018 mjini Geita, Bashiru amesema Lowassa ambaye kwa sasa ni mwanachama wa Chadema, hajawahi kuzusha wala kutoa kauli mbaya dhidi ya Rais John Magufuli.

Kauli hiyo ya Dk Bashiru ni mwendelezo wa vita yake na Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akimtaka afike ofisini kwake kujieleza.

Alitoa kauli hiyo kwa mara ya kwanza akiwa mkoani Geita, akijibu ujumbe uliotumwa kwenye akaunti ya mtandaoni ya mtu mwenye jina la Bernard Membe kujibu tuhuma zilizotolewa na Dk Bashiru akiwa Geita.

Dk Bashiru alimtuhumu Membe kuandaa mpango wa kumkwamisha Rais John Magufuli katika uchaguzi wa rais na kwamba tangu ateuliwe hajawahi kuonana na mbunge huyo wa zamani wa Mtama.

Katika akaunti hiyo ya kwenye mitandao, Membe alieleza kushangazwa na utaratibu uliotumika kumuita akibainisha kuwa pengine ni ugeni wa kazini wa Bashiru, lakini akaahidi kwenda kumuona akirudi safari ya nje ya nchi.

Jana Dk Bashiru ameendeleza vita hiyo akiwataka wanasiasa wachanga na wa kati, akiwemo Membe kujifunza hekima na busara za Lowassa.

Amesema anamheshimu Lowassa kwa uamuzi wake wa kuondoka CCM baada ya kutopewa ridhaa ya kugombea urais na kwenda chama kingine badala ya kubaki ndani ya chama tawala kinafiki na kuwagawa wanachama

Amesema mtu kubaki ndani ya CCM kinafiki na kuendelea kugawa chama kwa makundi hawezi kumvumilia na atahakikisha anamaliza makundi kwenye chama hicho.

Amesema hayupo tayari kuona migogoro iliyowakumba makatibu wakuu waliomtangulia wakati wa uchaguzi akutane nayo sasa na kwamba mkakati wake mkuu ni kuua makundi.

“Sina shida na Lowassa aliko namheshimu huyu ni waziri mkuu mstaafu,” amesema Bashiru.

Soma zaidi:

Dk Bashiru ataja korosho akimshukia tena Membe

Membe, Dk Bashiru ngoma bado nzito

Share.

About Author

Leave A Reply