Thursday, February 21

Diamond azindua tamasha la Wasafi, ‘amuomba’ Alikiba ashiriki

0


Dar es Salaam. Kampuni ya Wasafi imetangaza kuanza rasmi kwa tamasha la Wasafi Festival ambalo linatarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 24, mwaka huu mpaka Desemba mwisho ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 5, mkurugenzi wa kampuni hiyo, Naseeb Abdul maarufu  kama ‘Diamond Platnumz’, amesema kwa kuanzia tamasha hilo lenye kauli mbiu ya ‘Mchezo usiuchezee wewe Kabisa’ litafanyika mkoani Mtwara katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Diamond alitaja mikoa mingine itakayofuata kuwa ni Iringa ambapo litafanyika Novemba 30 na kufuatiwa na Morogoro na mikoa mingine itatangazwa hapo baadaye huku Nairobi likitarajiwa kufanyika Desemba 31 mwaka huu .

Amesema tamasha hilo mbali na kujumuisha wasanii wa ndani pia wataletwa wasanii wa nje ikiwemo kutoka nchini Nigeria na Marekani ambao wamekuwa wakifanya nao kazi kwa karibu.

Diamond, mkali wa vibao vya Mbagala, Sikomi, Baila na African Beauty amesema fedha zitakazopatikana katika tamasha hilo nyingine zitasaidia jamii ya mkoa husika ikiwemo kununua sare za wanafunzi katika shule na kutoa mitaji kwa wakina mama 200.

“Tunataka tamasha hili kila linapofika liwanufaishe wakazi wa pale si kwenda tu kuchukua hela zao na kusepa, na kwa kuanzia tutawasaidia kina mama,” amesema.

Kuhusu wasanii amesema wale wote wanaofanya vizuri hapa nchini watakuwepo huku akisema anatamani hata Ali Kiba naye awepo.

“Natamani kaka yangu Ali Kiba naye awepo na ninaamini uongozi wangu utaanza mazungumzo naye na huko alipo kama anafuatilia wasafi ajue tungehitaji uwepo wake, kwani inabidi tutoke kwenye muziki wa mabifu na tuingie katika kutengeneza hela na kuisaidia jamii inayotuzunguka,” amesema.

Share.

About Author

Leave A Reply