Monday, August 26

Dhamana 11 milioni kwa wizi wa biblia 500

0


Wanaume watatu wameshtakiwa nchini Kenya Jumatatu kwa wizi wa Bibilia 500 na kuachiwa kwa dhamana ya Sh500,000 za Kenya (Sh11 milioni). 

Wanaume hao, Reuben Rogoi Maina, John Mapesa Andulu na Josephat Gatheru wamekanusha mashtaka mawili ya wizi wa biblia kutoka kituo cha kutafsiri bibilia Upperhill, Nairobi.

Shtaka dhidi Maina na Andulu lilisema kuwa Mei 16, 2019 wakiwa na nia ya kulaghai walipokea Biblia 300 za News King James version na nyingine 200 za Good News International Version na kutoa hundi feki ya Sh920,000 kwa Faith Mawia Mulunga.

Hundi hiyo nambari 000076 ya Sh920,000 ilikuwa ilipwe na Benki ya Cooperative tawi la Masai Mall, kwa mujibu wa gazeti la Taifa Leo.

Andulu na Gatheru wanakabiliwa na mashtaka peke yao kuwa Mei 16 walikutwa na gari aina ya Toyota Fielder lenye rangi nyekundu likisafirisha Biblia hizo zenye thamani ya Sh680,000.

Washukiwa wamekanusha mashtaka dhidi yao na kuomba waachiliwe kwa dhamana. Ombi hilo halikupingwa na kiongozi wa mashtaka.

Kila mmoja aliamriwa awasilishe dhamana ya Sh500,000 za Kenya. Hakimu mkuu Francis Andayi aliamuru upande wa mashtaka uwakabidhi washtakiwa hao nakala za mashahidi waandae ushahidi wao.

Kesi hiyo itatajwa baada ya wiki mbili upande wa mashtaka ueleze ikiwa umewakabidhi washtakiwa hao nakala za ushahidi.

Share.

About Author

Leave A Reply