Thursday, August 22

Claryo: Kipa Stars, tumaini jipya kwa Amunike

0


By Thomas Ngitu, Mwanachi

Kocha wa timu ya Taifa Tanzania Emmanuel Amunike amefanya uamuzi sahihi kwa kuonyesha dhamira ya kuinua vipaji vya wachezaji chipukizi, baada ya kumuita kinda Claryo Boniface katika kikosi chake kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon).

Pia Amunike amemuita kinda mwingine Kelvin John, katika kikosi cha wachezaji 39 ambao watachujwa na kubaki 23 watakaokwenda Misri kwa fainali hizo zilizopangwa kuanza Juni 23 hadi Julai 19.

Claryo na Kelvin ndio wachezaji pekee wenye umri walioitwa Taifa Stars kwa michuano hiyo na Fainali za Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN).

Katika maelezo yake, Amunike alisema lengo la kuwaita chipukizi hao ni kutaka kuwajengea uwezo na kupata uzoefu wa mashindano ya kimataifa.

“Hawa ni wachezaji walionivutia ingawa wapo wengi, nimewaita Taifa Stars ili wajifunze kitu kupitia kwa kaka zao, naamini ni vijana hodari wenye uwezo mzuri,” alisema Amunike.

Endapo Claryo atapenya katika orodha ya wachezaji watakaokwenda Misri atacheza pembeni ya kipa namba moja wa Taifa Stars, Aishi Manula anayecheza klabu ya Simba.

Kitendo cha kinda huyo kuitwa Taifa Stars kinaweza kufungua milango kwake kuendeleza kipaji chake na endapo atafuata maadili ndani na nje ya uwanja bila shaka atakiwa kipa hodari nchini.

Claryo anaweza kutamba kama ilivyokuwa kwa nyota wa zamani akina Omari Mahadhi, Idd Pazi, Athumani Mambosasa, Sahau Kambi, Joseph Fungo, Kichochi Lemba, Madata Lubigisa na wengine wengi tu, endapo atacheza mpira kwa nidhamu.

Spoti Mikiki ilizungumza na Claryo kuhusu mipango na mikakati yake ya soka baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuitumikia timu ya Taifa akiwa mchezaji mwenye umri mdogo.

Claryo anasema ilikuwa bahati ya mtende kuitumikia timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’ kwa kuwa jina lake halikuwahi kuchomoza katika soka.

“Nilikuwa nacheza katika akademi kule Mwanza, niliposikia kuna watu wanatafuta wachezaji nilienda kujaribu bahati yangu na nilifanikiwa kupita baada ya kuonyesha kiwango kizuri,”anasema Claryo.

Hata hivyo, kinda huyo hakudumu katika kikosi hicho kwani alitolewa baada ya kupitishwa mchujo na moja kwa moja alipelekwa timu ya Taifa ya vijana chini yaa miaka 18 ‘Ngorongoro Heroes’.

Claryo anasema ana deni kubwa kwa Amunike na Watanzania baada ya kuitwa kuitumikia timu ya Taifa katika mashindano ya kimataifa.

Mchezaji huyo anasema haijalishi kama atakuwemo katika safari ya kwenda Misri au vinginevyo, lakini kitendo cha kuitwa Taifa Stars ni heshima kubwa kwake.

Anasema baada ya kupata taarifa za kuitwa Taifa Stars alishituka kwa sababu hakuamini kama Amunike amemuona ana uwezo kuwazidi makipa wengine wakiwemo wakongwe.

“Naamini mwalimu ameangalia uwezo na umbo langu ndio maana amenipa nafasi ya kujifunza na kuanza maisha mapya katika soka,” anasema kinda huyo.

Claryo anasema pamoja na kuitwa timu ya Taifa, ana kibarua kigumu kuthibitisha uwezo wake mbele ya Amunike na makipa wakongwe akiwemo Manula.

“Changamoto itakuwepo kikubwa ni kupambana mimi ni kijana mdogo sana kwao kiumri na uzoefu pia kwahiyo naamini nitajifunza kupitia kwa wakubwa zangu,”anadokeza kinda huyo.

Chipukizi wengi wana ndoto ya kuzitumikia Simba, Yanga na sasa Azam, lakini kwa upande wa kipa huyo ana mtazamo tofauti kuhusu mustakabali wake wa soka hapo baadaye.

“Mpira ndio kazi yangu timu yoyote ambayo nitadhirika nayo kimasilahi nitacheza jambo la msingi ni maelewano kwasababu nisingependa kuingia katika mzozo usiokuwa na sababu katika usajili wangu,” anasema Claryo.

“Natambua idadi kubwa ya makipa Tanzania hawana ndoto ya kucheza Ulaya, lakini mimi nataka kuweka rekodi,” anasema Claryo.

Share.

About Author

Leave A Reply