Thursday, August 22

Chama cha mawakala wa forodha wapeleka kilio chao kwa Waziri Mkuu

0


By Happy Lazaro, Mwananchi. [email protected]

Arusha. Chama cha Mawakala wa Forodha (Taffa), tawi la Namanga, wamemwomba Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa kuingilia kati mgogoro baina yao na Wakala wa Vipimo (WMA).

Kimesema wakala huo unawalazimisha kulipia  tozo mpya inayotozwa kwa kila bidhaa badala ya kutumia utaratibu wa awali wa kulipia tozo kwa mzigo wote.

Chama hicho kimesema kipo tayari kufanya kazi na WMA hadi watakapoonyeshwa sheria mpya inayowalazimika kuitekeleza bila kuwepo kwa makubaliano yoyote.

Msimamo huo umetolewa jana Jumanne Mei 28, 2019 katika kikao kilichoongozwa na mwenyekiti wa tawi hilo, Ismail Lukas na kufanyika Namanga, wilayani Longido.

Wamebainisha kuwa walikuwa wakitumia sheria ya zamani ya mwaka 2016 ambayo inaelekeza walipie asilimia 0.2 ya thamani ya mzigo huku kiwango  cha chini cha malipo kikiwa Sh100,000 kwa mzigo.

Wamesema wanachopinga ni WMA kuamua kuwatoza malipo ya Sh100,000 kwa kila  aina ya bidhaa badala ya mzigo mzima Kama sheria inavyoelekeza .

Naye Meneja wa Tawi wa Kampuni ya EDPAC, Wilson Mkanza amesema kwa sasa hivi hawapo tayari tena kufanya shughuli yoyote bila kupata mwongozo wa sheria mpya inayowalazimu wao kutumia utaratibu mpya wa kulipa tozo ya laki moja kwa kila bidhaa, badala ya mzigo kama utaratibu wa awali. 

Amesema walipokea barua Mei 15, mwaka huu ya ufafanuzi wa kanuni za ada za ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa zinazoingia nchini kutoka nje ya nchi, kutoka kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo mkoa, Dismas Maturine inayohusu wao kulipia bidhaa moja badala ya kutozwa kwa mzigo mzima kama ilivyokuwa hapo awali bila kushirikishwa chochote kabla ya kupewa barua hiyo. 

Naye Janeth Mero kutoka Kampuni ya Beam Tanzania Ltd, amesema uwepo wa utaratibu huo wa kulipa kwa mzigo mmojammoja unatengeneza mazingira ya rushwa, hivyo kuwataka kuendelea na utaratibu wa awali.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi kutoka Wakala wa vipimo makao makuu, Stella Kahwa amesema watayafanyia kazi malalamiko na utaratibu utaendelea kutumika ule wa awali.

Share.

About Author

Leave A Reply