Tuesday, August 20

Chama cha makandarasi chaiomba Serikali kurejesha imani kwao

0


By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Chama cha makandarasi wazalendo (ACCT) kimeiomba Serikali kurejesha imani dhidi yake huku wakiitaka kuwachukulia hatua wachache wanaochafua jina la makandarasi wa ndani.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Aprili 24, 2019 katika mkutano wa mwaka wa chama hicho ambao umefanyika jijini hapa.

Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa ACCT, Milton Nyerere, amesema chama kinaiomba Serikali irejeshe imani na ijikite kuwasaidia makandarasi wa ndani kuliko kuwalaumu kwani uimara wao utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa.

“Kwa bahati mbaya sisi tukifanya vizuri huwa hatupongezwi ila tukiharibu huwa tunalaumiwa. Hata hivyo, asilimia zaidi ya 70 ya miundombinu yote  nchini imefanywa na makandarasi wa ndani sio yote ni mibaya au iko chini ya kiwango kuna mingine ni mizuri mpaka leo, hivyo tuaminiwe tu,” amesema Nyerere.

Akitoa mfano, amesema miradi mingi ya maji ambayo haijawa na ufanisi ni kwa sababu mfumo wa mradi wenyewe na sio tatizo la mkandarasi.

“Mradi unaweza ukakamilika lakini ukawa hautoi maji, tatizo sio la mkandarasi bali yeye amepewa mchoro wa kutekeleza ili hayo yasiwe yanatokea mkandarasi apewe zabuni kamili afanye utafiti na usanifu mwenyewe na kazi za kikandarasi afanye mwenyewe,” amesema.

Nyerere ameitaja changamoto nyingine kuwa ni sheria ya ununuzi ambayo sasa wenye zabuni wamekuwa wanataka mradi uwekewe dhamana benki tu na wakati sheria inaruhusu benki au bima, hivyo makandarasi wanashindwa kutekeleza miradi mingi kwa wakati mmoja kwa kuwa hawana mali za kuweka dhamana benki.

“Bima unalipia tu kiasi fulani kwa ajili ya mradi fulani lakini benki lazima uweke dhamana wakati huohuo hiyo dhamana ulitaka uichukulie mkopo wa kutekeleza mradi huo, inakuwa kitendawili  ukizingatia kuwa miongoni mwa changamoto tulizonazo makandarasi wa ndani ni ufinyu wa mitaji,” amesema Nyerere.

Msajili wa bodi ya makandarasi wa zamani, Boniphace Muhegi ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Ushauri ya JMK International Consultants, amewaambia makandarasi katika mkutano huo kuwa huu ni wakati mwafaka kwao kufanya ushirika ili waweze kupata zabuni kubwa na kuzitendea haki.

Amesema changamoto nyingine zipo kwa mkandarasi mmoja mmoja hivyo wanapaswa kuimarisha chama chao ili kuwa na kauli moja yenye nguvu ndipo Serikali itaweza kuwasikiliza.

“Endeleani kusajili wanachama wapya ili muwe wengi zaidi, mkiongea kwa sauti moja Serikali itawasikiliza lakini pia mzingatie kuwa jukumu la Serikali ni kutatua changamoto za wananchi kwa haraka na ubora,” amesema.

Share.

About Author

Leave A Reply