Friday, August 23

BLOOD BROTHERS Wanatembelea nyota za kaka zao Ligi Kuu

0


Dar es Salaam.Kuna hadithi mbalimbali za kusisimua kuhusu familia za wanamichezo duniani, na Tanzania ni hivyo hivyo.
Tumeshuhudia familia za wanamichezo kama ya familia iliyotoa mabondia kibao ya Rashid Matumla na nduguze kina Mbwana Matumla, Hassan Matumla hadi mtoto wa Rashid, Mohammed Matumla.
Lakini Mungu ni mkubwa, licha ya nyota hawa kutoka katika familia moja, hawalingani vipaji. Kama ilivyo kwa vidole vya mkono wako, licha ya kuumbwa katika mkono mmoja, havilingani  – kuna gumba, cha pete na kadhalika.
Katika soka la Bongo, hawa hapa ni watoto wa familia moja:  

SAIMON MSUVA vs JAMES MSUVA
Wamekua pamoja na wote ni wapenda soka, lakini Saimon ndiye aliyeanza kutoboa baada ya kutua Yanga na kucheza kwa mafanikio makubwa huku akijaribu kuushawishi uongozi wake wa Yanga umbebe mdogo wake acheze timu ya vijana. Alifanikiwa, lakini mdogo mtu hakuwa na mafanikio katika kikosi hicho cha vijana na kuamua kuachana nao.
Saimon Msuva sasa anacheza soka la kulipwa nje ya nchi katika klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco wakati mdogo wake James Msuva anakipiga katika klabu ya KMC, ambako pia alianza vibaya katika klabu hiyo akitokea Mbao kutokana na kusumbuliwa na majeraha. Licha ya kuanzia benchi, amefunga katika kila mechi aliyocheza. Ana mabao 5.

MOHAMMED SAMATA vs MBWANA SAMATA
Hapa sasa ni patamu na ni ngumu kwa ndugu hawa wawili kukutana katika uwanja mmoja kwani mdogo anazidi kupaa kimataifa kutokana na kuwa na kipaji zaidi tofauti na kaka yake anayekipiga katika klabu ya Mbeya City jijini Mbeya.
Mbwana anayekipiga katika KRC Genk ya Ubelgiji ndiye anayeongoza kwa upachikaji mabao katika ligi miongoni mwa Waafrika wanaocheza soka katika ligi za Ulaya hivi sasa akiwa amefunga mabao 20 wakati kaka yake anacheza klabu ya Mbeya City na hana umaarufu licha ya kuwa na mchezo mzuri awapo uwanjani.

DANNY LYANGA vs AYUB LYANGA
Jina la Lyanga siyo geni katika soka la Bongo. Limepaishwa na Danny kutokana na kucheza kwa mafanikio nchini katika klabu ya Simba msimu wa mwaka 2015 kabla hajatimka kwenda kujaribu maisha nje ya nchi na sasa amerudi tena anakipiga katika klabu ya Azam FC.
Wakati Danny akikipiga Azam FC unaambiwa ana mdogo wake anauwasha moto Coastal Union, Ayub Lyanga, ambaye naye anacheza nafasi hiyo hiyo ya ushambuliaji kama kaka yake. Huu ni msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya Bara na amekuwa tegemeo katika safu ya ushambuliaji ya Coastal.

HASSAN DILUNGA vs SAID DILUNGA
Simba inashuhudia ‘shughuli’ ya Hassan Dilunga mwenye pasi za kiwango cha ‘HD’ pale kwenye dimba la kati la mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Bara. Mashabiki wa Msimbazi wanakumbuka ‘pasi ile ya kifo’ aliyopiga katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nkana, ambayo ilizaa bao wakati Simba wakifuzu kwenda hatua ya makundi kwa ushindi wa 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Desemba 23 mwaka jana.

Achana na huyo HD, njoo huku Ruvu Shooting, utakutana na Said Dilunga. Yeye huyu hana jina kubwa, lakini anachokifanya uwanjani makipa na mabeki wa timu pinzani wanakifahamu. Kufikia sasa keshatupia kambani mabao 10 na ndiye mshambuliaji anayeongoza kwa upachikaji wa magoli katika kikosi hicho cha maafande.

RENATUS AMBROS vs AGREY MORIS
Renatus Ambros ni mchezaji wa zamani ambaye ni wachache sana wanaweza kumfahamu kutokana na soka lake kulicheza zaidi Zanzibar tofauti na Agrey Moris ambaye anakipiga katika klabu ya Azam FC kwa sasa na ndiye nahodha akidumu kwa muda mrefu pia akiwa na mchango mkubwa katika kikosi hicho.
Agrey ni beki tegemeo wa timu ya Taifa ya Tanzania na Azam FC, na ni mmoja wa wachezaji ambao wanajua kuwasoma wapinzani wao na anaogopwa na washambuliaji kutokana na kutokuwa na masihara awapo katika nafasi yake hiyo ya ulinzi.

Share.

About Author

Leave A Reply