Thursday, August 22

Beki Gadiel wa yanga aibua mzozo wa gari la wagonjwa

0


By Khatimu Naheka

Dar es Salaam. Beki wa kushoto wa Yanga, Gadiel Michael amezusha utata na kuwatibua mashabiki wa timu yake baada ya gari la wagonjwa kukosekana kwa muda.

Gadiel aliumia dakika ya 36 ya mchezo kati ya Azam dhidi ya Yanga kisha nafasi yake kuchukuliwa na Jafary Mohammed dakika ya 38.

Baada ya kutolewa Gadiel alipelekwa moja kwa moja chumba cha huduma ya kwanza akionekana kuwa na maumivu makali ya kifundo cha mguu wake wa kulia.

Wakati timu zikiwa katika mapumziko Gadiel alionekana kutolewa kwa msaada wa watu wa huduma ya kwanza wakimshika kulia na kushoto wakimtoa nje tayari kwa kukimbizwa hospitali.

Hata hivyo, wakati beki huyo akifika nje ya geti la kuingilia vyumbani changamoto ya gari la wagonjwa ikajitokeza kwa gari kutokuwepo.

Wakati Gadiel akipumzishwa chini hatua hiyo iliwakera baadhi ya mashabiki wa Yanga na kuanza kutoa lawama kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na bodi ya ligi kwa kutokuwepo kwa gari la wagonjwa hali ya kuwa katika makato ya mapato viwanjani huduma hiyo hukatwa fungu maalum.

Hata hivyo wakati mashabiki hao wakitafuta usafiri binafsi kumkimbiza hospitali beki huyo ghafla gari ya wagonjwa ilifika na kumaliza utata huo na Gadiel kukimbizwa hospitali.

Share.

About Author

Leave A Reply