Monday, March 18

Aussems: Msihofu, tunawapiga na huku

0


By Khatimu Naheka

SIMBA imefanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo wa leo dhidi ya Mbabane Swallows, lakini kocha wao Patrick Aussems amesema wamekuja kutafuta ushindi sio kujilinda.

Amewataka mashabiki wa Simba kuendelea kutembea vifua mbele kwani, ushindi kwenye mchezo huo ni lazima na kuwa dhamira ya kusonga mbele kwenye hatua inayofuata iko pale pale na hakuna tishio la matokeo kupinduliwa.

Simba ilitua jijini Manzini kwa mafungu na kufanya mazoezi ya kwanza juzi, lakini jana pia walifanya mazoezi katika Uwanja wa Mavuso.

Katika mazoezi ya jana, wachezaji wa Simba walionekana wakiwa na morali kubwa kuelekea mechi hiyo huku wakifurahishwa na ubora wa uwanja.

Beki mkongwe wa Simba, Erasto Nyoni alisema kwa hali ya Uwanja wa Mavuso wana kila sababu ya kufanya vizuri kutokana na kuwa na nyasi kama za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa Mavuso ambao, unachukua mashabiki 7,500 waliokaa ukiwa na nyasi za kawaida.

Faida kubwa ya uwanja huo kwa Simba ni kwamba, kutokana na mchezo huo kupigwa siku ya kazi hautawavuta mashabiki wengi wakitarajia kupata mashabiki 4,000.

Meneja wa Uwanja wa Mavuso, Mangaliso Mkhatjwa amesema sababu nyingine ambayo itawapunguza mashabiki ni ushindi mkubwa ambao, wageni wao waliupata katika mchezo wa kwanza. Ushindi huo umewavunja moyo mashabiki wengi wa Swallows.

“Tunataraji mashabiki watakuja ingawa sio kwa idadi kubwa kutokana na mchezo kuchezwa siku ya kazi. Pia matokeo yaliyopita yalitibua mashabiki.” alisema Mkhantjwa.

Katika mchezo huo utakaoanza saa 9:00 alasiri ikiwa ni saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, Aussems amesema hawakuja kupaki basi wakiwa hapa.

Aussems amesema ingawa kutakuwa na mabadiliko madogo katika mfumo wa uchezaji lakini hafikirii kubadilisha kikosi chake sana.

Alisema walichokubaliana na wachezaji wake ni kusahau matokeo ya mchezo wa kwanza lakini hatapunguza idadi ya washambuliaji wake.

Alisema wanatambua kwamba katika mchezo wa kwanza timu zote zilifanya baadhi ya makosa na kwamba wao watayafanyia kazi mapungufu ya wapinzani wao.

“Hakuna majeruhi kwa wachezaji wote waliopo hapa nafurahi kuona maandalizi ya timu tangu yako sawa.

“Hatuwezi kupunguza washambuliaji ili tujaze mabeki tukifanya hivyo itakuwa ni sawa na kuwaambia wapinzani watushambulie.”

Kutokana na mapungufu ya mchezo wa kwanza Aussems amesema sehemu pekee inayompa wasiwasi ni kule kwa beki wa kulia Nicholas Gyan.

Amesema kuumia kwa beki Shomari Kapombe kumefanya wamtumie Gyan na hata hivyo, wamehakikisha hakutakuwa na matatizo.

“Tangu tulivyoanza ligi nilijua kwamba kuna siku litatokea tatizo la namna hii, hata hivyo namuamini Gyan na tutahakikisha tunakuwa na wakati mzuri.”

Ikifanya mazoezi katika Uwanja wa Mavuso Aussems akificha sura ya kikosi chake, amekuwa akisisitiza pasi za uhakika, kukaba kwa akili nje ya eneo la hatari.

Mbali na hilo Aussems amekuwa akipambana kuhakikisha wanatengeneza nafasi nyingi za kufunga huku pia washambuliaji wakifunga bila kupoteza.

Katika zoezi hilo washambuliaji Emmanuel Okwi na John Bocco walionekana kuwa na ubora katika kufunga huku Meddle Kagere akifuatia.

Share.

About Author

Leave A Reply