Tuesday, August 20

Askofu Nzigilwa: Kifo si mwisho wa maisha

0


By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa amewakumbusha waumini kwamba kifo si mwisho wa maisha yao bali kuna maisha mengine baada ya hapa duniani.

Askofu Nzigilwa ameyasema hayo leo Aprili 21 wakati akiongoza ibada ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Joseph lililopo jijini Dar es Salaam.

Amesema Sikukuu ya Pasaka ni kumbukumbu ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo ambaye kupitia kifo chake kilichotokea zaidi ya miaka 2000 iliyopita, ulimwengu ulikombolewa.

“Kifo si mwisho wa maisha ya Mkristo na kaburi si nyumba ya milele ya Mkristo kama tunavyoambiwa. Yesu alisema anakwenda kwa baba kuandaa makao ili atakapokuwa nasi tuwepo.”

“Sasa yeye hayupo tena kaburini, alifufuka. Alishinda kifo na mauti, ndiyo maana leo tunakumbuka ufufuko wake. Hilo ndiyo fumbo la imani yetu Katoliki,” amesema Askofu Nzigilwa.

Amewataka Wakristo wawe wakarimu kwa watu wenye shida kwa kujitoa kusaidia wengine hata kwa vitu ambavyo wanavihitaji katika maisha yao.

“Pasaka itusaidie kutoka kwenye maisha ya zamani ya dhambi na kuanza maisha mapya yanayompendeza Kristo mfufuka,” amesema Askofu Nzigilwa kwenye ibada hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya waumini.

Baadhi ya waumini wa kanisa hilo wamefurahi kuanza kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa ibada takatifu kwa sababu itawafanya watafakari maisha yao ya kiroho na kutenda yaliyo mema.

“Unajua siku kama ya leo, sisi vijana tuna mambo mengi. Lakini ukianzia kanisani unapata ile hofu ya Mungu, kwa hiyo kama ulikuwa umepanga kufanya mabaya, hufanyi tena,” amesema Oscar Tembo, muumini wa kanisa hilo.

Share.

About Author

Leave A Reply