Sunday, August 18

Askofu awaasa Watanzania kuwa macho na umwagaji damu

0


By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Dk Benson Bagonza amewataka waumini na wananchi kwa ujumla kuwa makini na umwagaji damu usio na hatia.

Dk  Bagonza ameyasema hayo leo Aprili 19, 2019 kwenye ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kitaifa katika kanisa la KKKT dayosisi ya Karagwe Usharika wa Kanisa Kuu Lukajange.

Amesema damu ya mwenye haki haimwagiki bure, isipokomboa inaangamiza, kwa sababu ya kutukuza, kushabikia, kushiriki, kukumbatia, kukalia kimya au kukumbatia umwagaji wa damu isiyo na hatia kuna madhara kwa waliopo na vizazi vinne vijavyo.

“Hii  ni kwa mujibu wa biblia,” amesema Askofu Bagonza.

Amesema unaweza usiangamie wewe unayeshiriki, kutukuza, unayekalia kimya na kushabiki ukaja kuangamia uzao wako au taifa lako, ilhali wao hawana hatia kwa sababu hawakuwepo wakati unatenda jambo hilo.

Amesema tendo hilo la mateso na kufa mwokozi Yesu Kristo ndiyo msingi na imani ya dini ya Kikristo.

Amefafanua Kibiblia Petro alitaka kuzuia ukombozi wao hakutaka bwana Yesu aende msalabani.

“Sisi binadamu hatutaki mateso, ikibidi ni kuwatesa wengine badala yetu,” amesema.

Amesema unapomtesa mtu ni sawa na umetengeneza sanamu na kuiabudu kwa sababu Yesu aliteswa, ukifanya hivyo unamgeuza mtu huyo kuwa Yesu.

“Mara nyingi watesaji hawajui kwamba yule wanayemtesa wanamwabudu na kumgeuza sanamu yao ya kuabudu,” amesema Askofu Bagonza.

Amesema utesaji ni kama bangi ikishaingia mwilini yanaingia mazoea ya kutesa tesa watu na usipofanya hivyo unawashwa washwa, ndivyo walivyokuwa maaskari wa Kiyahudi wakati wa Yesu.

Ameeleza tendo lililomtokea Yesu siku zile bado linaendelea kusumbua imani ya watu wengi.

“Tendo hili linasimama katika misingi mikuu miwili ya kibiblia ni upendo kwamba Mungu aliupenda ulimwengu na watu wake akamtoa mwanaye wa pekee Yesu Kristo afe awe sadaka badala, kwa niaba na kwa ajili yetu.”

“Badala ya sisi kufa kwa ajili ya dhambi zetu tulizozitenda Yesu afe, asimame kwa niaba yetu afe,” amesema.

Share.

About Author

Leave A Reply