Monday, July 22

Askofu aomba Serikali kusaidia wenye vipaji

0


Same. Askofu wa Jimbo Katoliki la Same, Rogath Kimario ameiomba Serikali iangalie namna ya kuwasaidia wanafunzi wenye vipaji maalum ambao wanaishi katika mazingira magumu.

Askofu Kimario ametoa ombi hilo leo Jumapili Novemba 18, 2018 wakati wa mahafali ya tatu katika shule ya Sekondari ya Wavulana ya Mtakatifu Joackim iliyopo Same. Jumla ya wanafunzi 95 wamehitimu masomo yao ya kidato cha nne.

Amesema vijana wengi wenye vipaji maalum, vipaji vyao vimekufa kutokana na kukosa watu wa kuwasaidia na kuwaendeleza hivyo vipaji vyao vinapotea bila kujali kuwa wao ndiyo nyenzo muhimu ya kufanikisha sera ya uchumi wa viwanda.

“Serikali iangalie uwezekano wa kuwasaidia wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu kwani wengi wao ndoto zao zimekufa kutokana na kukosa msaada, wakisaidiwa vyema watakuja kuwa msaada mkubwa kwa Taifa hili,” amesema.

Pia amesema kuwa jimbo hilo limeamua kuanzisha mfuko wa maendeleo ya elimu jimbo kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu na yatima.

“Ili Serikali iendane na sera ya viwanda, inatakiwa isaidie hawa vijana wenye vipaji maalum kwa ajili ya kuja kulisaidia Taifa hapo baadaye. Taifa hili linahitaji vijana mahiri ili kuendana na misingi ya sayansi na teknolojia,” amesema Askofu Kimario.

Kwa upande wake mkuu wa shule, Padre Deogratius Mchagi amesema Tanzania ya viwanda inahitaji kuandaa vijana wenye utaalamu mkubwa na nidhamu ya kutosha katika kazi.

“Nchi yetu kwa sasa tunasisitiziwa ni Tanzania ya viwanda lakini Tanzania ya viwanda haiwezekani bila kuandaa wataalam,” amesema mkuu huyo wa shule.

Hata hivyo, wanaiomba Serikali iangalie namna ya kupunguza gharama za vifaa vya kufundishia vya mazoezi ya sayansi kwani gharama zake ni kubwa sana na kwa nchi ya viwanda kuna umuhimu wa kufanya upatikanaji wa vifaa vya kufundishia kuwa rahisi.

“Ili serikali yetu ipate wataalam wazuri na waliopikwa na wenye ujuzi mzuri ni lazima wasome shule bora zenye vifaa vya kisasa vya kutosha vya kufanyia mazoezi ya vitendo,” amesema

Lukananze Romani, ambaye ni mwanafunzi aliyehitimu kidato cha nne katika shule hiyo, amewataka wanafunzi wenzake kutokata tamaa na badala yake watafute wafadhili kwa nguvu zote ili wafikie malengo yao.

Share.

About Author

Leave A Reply