Monday, March 18

Arsenal yafikisha mechi 19 bila kilio

0


London, England. Arsenal iliendeleza wimbi la ushindi ilipoichapa Tottenham kwa mabao 4-2, lakini jambo kubwa ni kwamba ikifikisha mchezo wa 19 mfululizo bila kupoteza.

Ushindi huo kwenye Uwanja wa Emirates umekifanya kikosi hicho cha kocha Unai Emery, kutinga hatua ya nne bora kwa mara ya kwanza ikiishusha Tottenham kwa wastani wa mabao zote zikiwa na pointi 30.

Kikosi hicho kimepata ushindi huo muhimu takribani wiki mbili tangu aliyekuwa kocha wake wa zamani, Arsene Wenger, aliposema timu hiyo imerejea kwenye ubora wake.

Wenger ambaye aliondoka mwishoni mwa msimu uliopita baada ya mashabiki kuchoshwa na timu kukosa mafanikio chini yake akiwa ameiongoza timu hiyo kwa miaka 22, alisema anauona mwanga wa mafanikio kwa mrithi wake.

Akizungumza kiwango cha vijana wake katika mchezo wa jana uliochezwa kwenye Uwanja wa Emirates, dhidi ya mahasimu wao wa London Kaskazini, Emery alisema walicheza vema katika kipindi cha pili.

Alisema katika kipindi cha kwanza hawakutengeneza nafasi za kutosha lakini kipindi cha pili walifanya kile walichotakiwa kukifanya tangu mwanzo.

“Nadhani kwa sasa tumekuwa na hamasa ya ushindi kwa kile mchezo kama tutaendelea hivi itakuwa vizuri sana” alisema.

Emery alimfagilia mshambuliaji wake mahiri kutoka Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang aliyefunga mabao mawili katika mchezo huo mabao yaliyomfanya kuongoza mbio za kuwania kiatu cha dhdhabu.

Mshambuliaji huyo amefikisha mabao kumi ikiwa ni mabao mawili juu ya aliyekuwa kinara wa ufungaji wa kwa muda mrefu, Sergio Agüero anyelingana na mchezaji mwenzake wa Manchester City, Raheem Sterling na nahodha wa Tottenham, Harry Kane.

Kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino, alisema mchezo ulikuwa mzuri na kwamba wachezaji wake walipaniki jambo lililowatoa mchezoni na kuchangia kupoteza mchezo huo.

Alisema katika mchezo wa soka moja ya mambo yanayoweza kusababisha kupoteza mchezo ni hasira au presha ya kutaka bao kwa wachezaji.

Share.

About Author

Leave A Reply