Saturday, August 17

Angola: Tunaiheshimu Serengeti Boys ila dakika 90 zitaamua

0


By Charles Abel

Dar es Salaam. Katika kile kinachoonekana ni mbinu ya kucheza na saikolojia ya timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’, kocha wa Angola, Pedro Goncalves amesema anawapa heshima kubwa wenyeji katika mchezo wa kesho baina yao kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Angola wanahitajika kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo huku wakiombea Uganda itoke sare au ifungwe na Nigeria ili wakihakikishie kufuzu hatua ya nusu fainali na pia kukata tiketi ya kushiriki fainali za dunia kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Brazil.

Kocha wa Angola, Goncalves alisema pamoja na matokeo yasiyoridhisha ambayo Serengeti Boys iliyapata kwenye mechi mbili zilizopita, anaamini mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwao kutokana na ubora wa wapinzani wao.

“Serengeti Boys kupoteza mechi mbili zilizopita dhidi ya Nigeria na Uganda hakufanyi ionekane ni timu dhaifu na binafsi naamini ni moja ya timu bora na nzuri kwenye mashindano haya.

Tutaingia kwenye mchezo wa kesho tukiwapa heshima kubwa na kucheza kwa uangalifu wa hali ya juu ili tuweze kupata ushindi ambao utatuvusha kwenda hatua inayofuata.

Kiuhalisia bado nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali wanayo hivyo nadhani mechi haiwezi kuwa rahisi lakini lengo letu ni kupata ushindi.

Goncalves alisema hakuna timu isiyotamani kucheza hatua ya nusu fainali ya mashindano kama hayo kwani ina faida kwa nchi na mchezaji mmojammoja.

“Shabaha yetu kwa sasa ni kuingia hatua ya nusu fainali ambayo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya mchezaji kwani inampatia uzoefu wa kutosha na kumjenga kiuchezaji.

“Kwa kulitambua hilo, nimekaa na wachezaji wangu na kuwajenga kiakili ili waufikirie mchezo wa kesho ambao una umuhimu kwetu,” alisema Goncalves

Angola hata hivyo itaingia kwenye mchezo huo ikimkosa nahodha wake Jose Cabingano anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata katika mchezo uliopita dhidi ya Nigeria walipofungwa mabao 3-0.

Share.

About Author

Leave A Reply