Tuesday, August 20

Alliance waichimba mkwara Simba

0


By SADDAM SADICK

ALLIANCE FC imesema licha ya kasi waliyonayo Simba kwa sasa kwenye Ligi Kuu Bara, haiwaogopeshi na mechi yao ya Jumanne, Wekundu hao wasitarajie mteremko kabisa.

Simba ambayo ipo Kanda ya Ziwa kumalizia mechi zake, itashuka dimbani kuvaana na Alliance FC kesho Jumanne, mchezo ambao utapigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Simba inawakabili Alliance ikikumbuka kichapo kikali ilichokitoa kwa Vijana hao wa Mtaa wa Mahina mabao 5-1, mpambano uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Kessy Mzirai alisema benchi la ufundi linaendelea kuwaweka sawa nyota wao kwa ajili ya mchezo huo ili kushinda na kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo.

Alisema wanafahamu ushindani wa Simba, lakini hawatakubali kufungwa mara mbili isipokuwa watapambana kulipa kisasi na kujiwekea heshima.

“Hatupo nafasi nzuri katika msimamo, tunahitaji ushindi bila kujali ni timu gani tunacheza nayo. Simba ni timu kama zingine hivyo, tunataka ushindi na vijana wako tayari kwa kazi,” alisema Mzirai na kuongeza kwamba:.

“Kuna baadhi ya wachezaji ambao ni majeruhi kama beki Israel Patrick, lakini wamerejea katika ubora na maandalizi tunayoyafanya Simba hawataamini kitakachowatokea, hivyo niwaombe mashabiki wetu waje kwa wingi siku hiyo” alitamba Mzirai. Simba itavaana na Alliance baada ya kumalizana na Kagera Sugar mjini Bukoba jana.

Share.

About Author

Leave A Reply