Monday, March 18

Aga Khan waguswa kina mama

0


By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wataalamu, watafiti, walimu wa afya na wadau wa maendeleo takriban 100 kutoka mataifa mbalimbali wamekutana katika kongamano la kujadili afya ya wanawake wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na changamoto zinazowakabili.

Kongamano hilo limeandaliwa na Chuo cha Aga Khan kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (Muhas), Hospitali ya Aga Khan, Chuo Kikuu cha Udaktari Bingwa cha Aga Khan na wawakilishi wa Wizara ya Afya.

Akizungumza katika kongamano hilo, mkuu wa Chuo Kikuu cha Udaktari Bingwa cha Aga Khan tawi la Dar es Salaam, Profesa Hussein Kidanto alisema lengo ni kujadili afya ya mama hasa ukizingatia Tanzania haijafanya vizuri kwenye Malengo ya Milenia kwenye sekta hiyo.

Prifesa Kidanto alisema kuwapo kwa tatizo la vifo vya wajawazito na mimba za utotoni nchini, ni sababu zilizowafanya kuandaa kongamano hilo kwa ajili ya kujadili hali hiyo ili kuwasaidia wanawake na watoto.

“Afya ya mama na mimba za utotoni ni tatizo, ndiyo maana tupo hapa na tumemwalika kaimu mkurugenzi wa idara ya watoto na vijana wa kwenye kongamano hili ili tujadiliane namna ya kupunguza matatizo haya,” alisema Profesa Kidanto.

Profesa Kidanto alisema mapendekezo na maoni yatakayotolewa katika kongamano hilo yatapelekwa serikalini kwa ajili ya utekelezaji ili kukabiliana na changamoto hizo.

Naye mkurugenzi wa uuguzi wa Hospitali ya Aga Khan, Lucy Ngwai alisema kongamano hilo litasaidia kutengeneza mbinu na mkakati utakaosaidia kupunguza vifo vya wanawake na watoto.

Akichangia kwenye kongamano hilo, kaimu mkurugenzi msaidizi afya ya uzazi na mtoto, kutoka Wizara ya Afya, Makuwami Mohamed alikisifu Chuo Kikuu cha Aga Khan kwa kuzalisha madaktari wanaotoa mchango mkubwa katika kuboresha sekta ya afya nchini.

Pia, Mohamed alisema kila wizara ina jukumu ya kushirikiana na wizara yake katika mapambano ya vifo vitokanavyo na uzazi.

Hivi karibuni, shule ya ukunga na uuguzi ya Chuo Kikuu cha Aga Khan iliendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo maofisa tabibu, wakunga na wauguzi 100 wa hospitali, vituo vya afya na zahanati za Serikali katika wilaya za Temeke na Ilala.

Share.

About Author

Leave A Reply