Monday, June 24

Afcon yampasua kichwa Msuva

0


By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Klabu ya Difaa El Jajida ya Morocco, Saimon Msuva amesema akili yake ipo katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019.

Msuva alisema anakuna kichwa  namna ya kuisaidia timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ katika fainali hizo.

Taifa Stars imepangwa Kundi C na timu za Senegal, Algeria na Kenya katika fainali hizo zitakazoanza Juni 21 hadi Julai 19.

Msuva alisema kundi hilo ni gumu kwa kuwa linaundwa na timu zenye uzoefu wa kutosha katika mashindano ya kimataifa, hivyo wanatakiwa kujiandaa kikamilifu ili kupata mafanikio katika fainali hizo.

“Nafasi ipo wazi kwa kila timu, kikubwa kwetu ni kuwa kitu kimoja, inawezekana tukafanya maajabu kama mwaka 1980 kule Zambia,” alisema Msuva.

Mchezaji huyo wa zamani wa Yanga mwenye mabao 13 katika mashindano ya Ligi Kuu Moroco, alisema ana matumaini Taifa Stars itafanya vyema endapo itapewa maandalizi ya kutosha.

Msuva alisema fainali za Afrika ni mashindano yenye hadhi na Tanzania inatakiwa kujipanga ili kwenda kutoa upinzani. Taifa Stars inashiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 39. Mara ya mwisho Taifa Stars ilicheza fainali hizo mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria.


Share.

About Author

Leave A Reply