Sunday, August 18

Aaah! Kigoma Sisters wamekubali yaishe tu

0


By MASOUD MASASI

KOCHA wa Kigoma Sisters, Daud Siang’a amesema mambo yamekuwa magumu msimu kwenye Ligi Kuu ya Wanawake kisha akatamka wazi kuwa kwa sasa anafukuzia kumaliza mashindano katika nafasi nne za juu. Amesema zile ndoto za kuwania ubingwa ni kama zimefutika kwa sasa.

Kigoma Sisters yenye maskani yake mkoani Kigoma, inashika nafasi ya sita katika msimamo ikiwa na alama 24.

Akizungumza na Mwanaspoti, Siang’a alisema msimu huu umekuwa mgumu hasa mzunguko wa pili hivyo, imewalazimu kupambana kuhakikisha wanashika nafasi nne za juu.

“Ligi imekuwa ngumu msimu huu na kikosi changu hakiko sawa na kilichobaki ni kupambana ili tumalize nafasi za juu kama tatu ama nne sio mbaya sana,” alisema Siang’a.

Alisema tatizo kubwa ambalo linamsumbua msimu huu ni safu yake ya ulinzi kuruhusu mabao ya kizembe hivyo, kuwafanya kupoteza michezo mingi.

“Mambo mengi yametugharimu ikiwemo safu yangu ya ulinzi kuwa na changamoto, kwa sasa nafanya marekebisho eneo la ulinzi. Pia, nimekuwa na majeruhi wengi kwenye kikosi changu, lakini tutakabiliana na changamoto hizo na tutakaa sawa,” aliongeza kocha huyo.

Pia, amewataka mashabiki wa mkoa wa Kigoma kuendelea kuwapa sapoti wachezaji wake kwa kujitokeza kwa wingi kuishangilia uwanjani leo Jumatatu watakapokipiga na Marsh Queens.

Share.

About Author

Leave A Reply