Wednesday, August 21

TGNP MTANDAO WAENDA SAMBAMBA NA AGIZO LA RC MAKONDA KWA DAWASCO.

0Hatimaye maneno aliyoyasema Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh. Poul Makonda yamejidhihilisha mapema jana katika semina za jinsia na maendeleo GDSS.

Baadhi ya wanaharakati wakifuatilia semina kwa umakini mapema jana makao makuu ya TGNP Mtandao Mabibo jijini Dar es salaam.

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Poul Makonda aliwataka wafanya kazi wa shirika la maji Dawasco kufanya kazi kwa weledi na kuacha tabia za kuwabambikizia wateja wao bili kubwa ambazo haziendani na maji waliyotumia.

Makonda aliyasema hayo tarehe 16 ya mwezi huu wa tatu alipokuwa akizindua maadhimisho ya wiki ya maji yaliyofanyika ukumbi wa Mwalimu JK. Nyerere uliopo posta jijini Dar es salaam.

Washiriki wa semina hiyo iliyofanyika mapema jana tarehe 21 walisema kuwa dawasco wamezidi kwa kuwawekea watu bili zisizokuwa zao kwa maslahi yao binafsi na hii inatokana na uzembe wa wasoma mita kwa kutoa taarifa za uongo.

Mmoja wa wanaharakati aliyeudhuria semina na hiyo bw. Hamisi Masanja alisema kuwa yeye aliletewa bili ambayo ilikuwa kubwa sana na aliamua kwenda mpaka kwa mkurugenzi wao na kubaini kuwa bili hiyo ilikuwa ni kubwa kiasi ambacho mpaka mkurugenzi alishangaa na kutoa ahadi ya kumuwajibisha aliyefanya kitendo hicho.

Katika mfurulizo wa Semina za jinsia na maendeleo ambapo wiki hii mada kubwa ilikuwa ni “huduma ya maji kwa usafi binafsi na mazingira ya mtoto wa kike na maendeleo yake kitaaluma”

Akiongoza semina hiyo Afisa sera wa Mtandao wa Asasi za maji na usafi wa mazingira Tanzania(TAWASANET) Bw. Darius Mhawi alisema kuwa maji ni muhimu kwa kila mwanadamu na ndio maana serikali imeichukua agenda hii ya kimataifa na kuiweka katika ngazi ya kitaifa.

“Inafahamika kuwa kila ifikapo tarehe 16 mpaka 22 mwezi wa tatu dunia nzima inaadhimisha siku ya maji duniani na kwa kuona umuhimu wa agenda hii serikali imeichukua na kufanya maadhimisho haya kila ifikapo tarehe hizo alisema” alisema Afisa Darius

Aliongezea kwa kusema kuwa serikali inajukumu la kuhakikisha kila mwananchi anapata maji safi na salama kwa matumizi yake ya kila siku, na ndio maana imeweka Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kuwa wizara hiyo inawataalamu mbalimbali wanaojua aina za maji na kujua watatumia miundo mbinu gani ili wananchi wote wapate maji.

Afisa Darius aliendelea kusema kuwa maendeleo ya watoto wakike yanategemea sana maji kwani yanapokosekana wao ndio wanaowajibika kuyatafuta hata kama yanapatikana kwa umbali mrefu, hivyo hali hii inasababisha kudumaa kwa maendeleo yao kitaaluma kwa upande wa elimu na hata katika maendeleo yao binafsi.

“Lakini pia hata mashuleni maji yanapokosekana huwa inawaathiri sana watoto wakike kwa kuwa wao hata wakienda haja ndogo wanalazimika kunawa kwa maji safi na hata wakiwa katika siku zao inabidi waende kujisafisha ili waendee kujisitili na taulo zao na kukosekana kwa maji inakuwa ni ngumu sana kwa hali yao” alisisitiza Darius

Baada ya mjadala huo baadhi ya wanaharakati walitoa maoni yao kuhusu umuhimu wa maji na nini kifanyike kuwakomboa watoto wa kike na wamama kwa ujumla ili kupunguza tatizo hili na maoni yao yalikuwa kama ifuatavyo.

Kuboresha miundo mbinu ya maji kwa maeneo ya vijijini ili kuwakomboa na maradhi mbalimbali kwani asilimia kubwa wananchi wa maeneo hayo hawapati maji safi na salama.

Serikali kuhakikisha huduma ya maji inapatikana mashuleni lakini pia kutoa taulo za kujihifadhia kwa watoto wa kike na vyumba vya kujihifadhia ili kuondoa tatizo la watoto wa kike kukosa masomo kwa siku kadhaa kwa sababu ya ukosefu wa vitu hivyo.

Lakini pia swala lingine kubwa limeonekana ni kuwepo kwa maji ya kutosha hasa katika zahanati za vijijini ili kuepusha tatizo la mama mjamzito kwenda na ndoo ya wakati wa kujifungua.

Na mwisho ni swala la miundo mbinu ya Maji taka kwani maeneo kama ya mjini watu wanashindwa kuhifadhi vizuri maji taka na kuyaachia pindi mvua inaponyesha na kwa hali hii inasababisha mlipuko wa magonjwa kama kipindu pindu.
Afisa Sera wa (TAWASANET) Bw. Darius Mhawi akitoa ufafanuzi wa jambo fulani kwa wanarakati mapema jana katika semina ya Jinsia na Maendeleo(GDSS) iliyofanyika Makao Makuu ya TGNP Mtandao Mabibo Dar es salaam.
Wanaharakati kutoka sehemu mbalimbali za jiji la Dar es salaam wakimsikiliza kwa umakini muwezeshaji.
Mzee Hamisi Masanja akitoa mchango wake katika semina ya jinsia na maendeleo iliyofanyika jana jijini Dar es salaam.
Semina ikiendelea.
Dada Anna Sangai akifunga semina baada ya muwezeshaji kumaliza kuwezesha.


Read More

Share.

About Author

Comments are closed.