Saturday, August 17

Vituo 15 vya mafuta vyatozwa faini, serikali yaeleza sababu

0


Vituo 15 vya biashara ya kuuza na kusambaza mafuta ya petroli Zanzibar vimetozwa faini kufuatia kufanya vitendo vya udanganyifu ikiwamo kuficha mafuta na kusababisha uhaba wa nishati hiyo.

Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Salama Aboud Talib, aliwaambia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wakati akitoa ufafanuzi kufuatia kujitokeza kwa tatizo la uhaba wa nishati hiyo katika kipindi cha wiki moja.

Alisema faini iliyotozwa kwa vituo hivyo inatokana na kuficha mafuta na kuyauza kwa bei ya ulanguzi.

Akifafanua zaidi alisema ni kweli ulikuwepo uhaba wa mafuta katika kipindi cha wiki moja ambao ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na kampuni ya mafuta ya Unite Petroleum, kukabiliwa na uhaba wa mafuta katika hifadhi yake.

Alisema upungufu huo ulichangiwa na kuchelewa kwa upakuzi wa mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam ambayo kwa sasa imeweka utaratibu mpya.

Hata hivyo, Talib alisema serikali imeziona changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika kutoa huduma ya nishati ya mafuta kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Mafuta Zanzibar (Zura).

Aidha, aliwatoa hofu wananchi kuwa kuna mafuta ya kutosha kwa matumizi mbali mbali ya wananchi wa Zanzibar huku akitoa onyo kali kwa kampuni zilizopewa leseni ya kutoa huduma hiyo kuacha kutumia mwanya wa upungufu wa mafuta na kuongeza bei kwa njia ya ulanguzi.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia Kamati ya Habari na Utalii, walisikitishwa na tatizo la kuwpo kwa uhaba wa nishati ya mafuta mara kwa mara ambalo ni moja ya kikwazo cha kuyumba kwa biashara ya sekta ya utalii.

 Read More

Share.

About Author

Comments are closed.