Friday, July 19

Milioni 50 za Rais Magufuli zimechangia Tanzania kufungwa goli 1- Waziri Mwakyembe

0


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe amesema kuwa, shilingi milioni 50 walizopewa na Rais Dkt Magufuli kwa ajili ya maandalizi ya Tanzania katika mechi dhidi ya Lesotho, zimechangia timu kufungwa goli moja.

Aliyesema hayo nchini Lesotho wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mchezo huo, ambapo Tanzania iliyaweka rehani matumaini ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2019 ambazo zitafanyika nchini Cameroon.

“Milioni 50 tulizopewa zimetusaidia kufungwa bao moja tu pengine tungefungwa hata sita,” alisema Waziri Mwakyembe na kuongeza kuwa, “ila tumefungwa sawa ndiyo mchezo tunaendelea kutafuta ushindi, tumejitahidi sana ila kwa sasa sio kichwa cha mwendawazimu tena.”

Kwa kuwa Rais alitoa fedha hizo akitaka timu hiyo irejee na ushindi, lakini sasa imefungwa, Waziri Dkt Mwakyembe amesema kuwa akifika Tanzania atamueleza Rais Dkt John Pombe Magufuli kuwa kilichotokea kwenye mchezo dhidi ya Lesotho kuwa ni bahati mbaya, na kumuahidi kuwa kwenye mechi dhidi ya Uganda, Taifa Stars itaibuka na ushindi.

“Rais alisema turudi na ushindi, nitamwambia tumefungwa moja na tunasubiri mechi ya Uganda ambayo lazima tushinde, huu ndiyo moyo wa kimchezo,  ukijikunyata utakuwa unadundwa ngumi kila wakati.”

Ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu fainali hizo mwakani, Tanzania ilitakiwa kupata ushindi dhidi ya Lesotho, ili iwe na alama nane, ikisubiri mchezo wake na Uganda utakaopigwa Machi 2019 jijini Dar es Salaam.

Kutokana na kufungwa huko, Tanzania sasa natakiwa kuhakikisha inaifunga Uganda, huku ikiiombea dua mbaya Lesotho ifungwe na Cape Verde. Au Tanzania iifunge Uganda kwa magoli mengi, ili hata Lesotho ikishinda na wakalingana alama (8), iweze kusonga mbele kwa utofauti wa magoli.

Nchi ambazo tayari zimefuzu hadi hivi sasa ni Cameroon, Misri, Madagascar, Mali, Morocco, Nigeria, Senegal, Tunisia na Uganda.

Comments

Share.

About Author

Leave A Reply