Tuesday, August 20

Kauli ya serikali baada ya kupokea bajeti ya maziko ya Akwilina

0


Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Leonard Akwilapo amesema, serikali itaangalia vitu vya msingi vya kugharamia kwa ajili ya mazishi ya mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), cha jijini Dar es Salaam.

Msichana huyo, Akwilina Maftah (22) alikufa kwa kupigwa risasi Februaroi 16 mwaka huu, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Familia ya Akwilina, imekabidhi serikalini bajeti ya Sh milioni 80 ya mazishi.

“Wao wameandaa bajeti hiyo lakini na sisi kama serikali tuna vitu vya msingi vya kugharamia ambavyo ni kama chakula, usafiri, jeneza na vingine,” amesema Dk Akwilapo.

Familia ya marehemu jana ilikabidhi bajeti hiyo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Leonard Akwilapo kwa utekelezaji kama ambavyo serikali iliahidi kugharamia msiba huo.

Msemaji wa familia, Festo Kavishe aliliambia gazeti hili jana kuwa familia imeandaa bajeti hiyo kwa ajili ya kufanikisha mazishi na kuikabidhi kwa serikali na kwamba watashukuru endapo watapatiwa fedha zote kama walivyoomba.

“Ni kama mtu umebeba ndoo mbili za maji, mtu akija akakupokea ndoo moja utashukuru, akikupokea ndoo zote mbili utashukuru zaidi, kwa hiyo na sisi hatuna namna serikali itakavyoamua kusaidia sawa,” alisema.

Alisema katika msiba huo watu wanaotarajiwa kusafiri na mwili kwenda kwenye maziko Rombo mkoani Kilimanjaro ni 300 ambao ni ndugu, jamaa na wanachuo waliokuwa wakisoma na Akwilina.

Mchanganuo wa bajeti hiyo ya familia unaonesha kuwa jeneza ni Sh milioni 1.5, malipo hospitali Sh 200,000, gari ya kusafirisha mwili Sh milioni 3, magari ya kusafirisha wafiwa makubwa matano Sh milioni 20, chakula njiani Sh milioni 3, chakula kwenye msiba Mbezi kwa siku tatu Sh milioni 10, viti 200 Sh 400,000.

Turubai kwa siku tatu ni Sh 600,000, mwongoza shughuli Sh 400,000, picha Sh milioni 1 na maji ya kutumia nyumbani Sh 50,000. Kwa pande wa Rombo, Kilimanjaro, chakula kwa siku tano ni Sh milioni 30, muziki na mwongoza shughuli Sh 200,000, turubai Sh milioni 1, viti Sh 400,000, kinywaji cha mabora Sh 100,000, kaburi la kisasa Sh milioni 3, maua na mataji Sh milioni 1, mapambo Sh 500,000 na dharura na tahadhari Sh milioni 2.

Kaka wa Akwilina, Moi Kiyeyeu alisema maziko yatafanyika kesho kutwa Rombo mkoani Kilimanjaro ambapo mwili wa Akwilina utaagwa kesho katika Chuo cha NIT Mabibo kuanzia saa 7 mchana.

Hata hivyo alisema jana jioni wangekutana na Kamati ya Msiba huo kujadili bajeti hiyo kwa kina na kuona kuwa huo ni msiba, hivyo kitu cha msingi si bajeti hiyo bali ni shughuli ya mazishi.

Februari 16, mwaka huu Akwilina alikuwa kwenye basi linalofanya safari zake Mabibo-Makumbusho lenye namba za usajili T 558CSX Nissan Civilian ambapo alipigwa risasi kichwani wakati gari hilo likiwa eneo la Mkwajuni, Kinondoni wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa katika maandamano.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.