Friday, March 22

Kampuni ya China kujenga awamu ya pili ya mradi wa mwendokasi

0


Dar es Salaam: Kampuni ya ujenzi kutoka nchini China, China Civil Engineering and Construction Corporation imeshinda zabuni ya ujenzi ya awamu ya pili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) utakaogharimu TZS bilioni 368 ($160 milioni).

Ujenzi wa mradi huo utakaokuwa na barabara zenye urefu wa 20.3km utajumuisha barabara 2 za juu zitakazokuwa na upana wa mita 24 na urefu wa mita 150, vituo vya mabasi 29, kumba cha kuongozea pamoja na karakana ya magari (garage).

Ujenzi wa mradi huo ambao utaanza mwezi huu unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36 (miaka 3).

Afisa Uhusiano wa Wakala wa BRT, William Gatambi aliliambia gazeti la The Citizen kuwa mradi huo utaanza baada ya kukamilisha ulipaji fidia kwa wakazi waliopo pembezoni mwa Barabara ya Kilwa.

“Hadi sasa tumewalipa watu 56 kati ya 105 wanaostahili kulipwa fidia,” alisema Gatambi.

Alisisitiza kuwa, wale ambao hawajalipwa fedha zao bado wanakamilisha taratibu za kufungua akaunti za benki ili fedha ziwekwe humo huku wengine wakikamilisha taratibu za kisheria, na kwamba hakuna zuio lolote la watu kutolipwa.

Wakati mradi huo ukigharimu TZS bilioni 368, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeridhia kutoka TZS bilioni 324 kufadhili mradi huo, huku serikali ya Tanzania ikitarajiwa kutoka TZS bilioni 44 zilizobaki.

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu jijini Dar es Salaam, serikali ilianza kuweka mipango ya mradi wa mabasi yaendayo haraka mwaka 2003.

Serikali ilitabiri kuwa, idadi ya watu katika jiji la Dar es Salaam itakuwa ni zaidi ya milioni 5 ifikapo mwaka 2015, na hivyo iliialika  kampuni kutoka Japan, Japan International Cooperation Agency kwa ajili ya kuweka mipango ya usafiri wa BRT mwaka 2008.

Mradi huo uliwekwa chini ya ofisi ya Waziri Mkuu na Wakala wa Usafiri wa Mwendokasi (DART) uliundwa kwa kupitia notisi ya serikali ya Mei 25 mwaka 2007.

Mradi wa mabasi katika jiji la Dar es Salaam ukikamilika utakuwa na urefu wa kilomita 130, ambapo utakuwa umegawanyika katika awamu sita.  Awamu ya kwanza ya mradi huo ilfadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) ambayo ilitoa TZS bilioni 414 ($180 milioni).

Comments

Share.

About Author

Leave A Reply