Wednesday, May 22

Burundi yaagiza kufungwa ofisi za Umoja wa Mataifa nchini humo

0


Serikali ya Burundi imeliagiza Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kufunga ofisi zake na kuondoka nchini humo ndani ya kipindi cha miezi miwili.

Burundi ilitoa notisi hiyo jana Jumatano ambayo ilieleza ofisi hizo zinatakiwa kufungwa ndani ya miezi miwili, na watumishi wote wa kimataifa kuondoka Bujumbura.

Nchi hiyo ilisitisha ushirikiano na ofisi ya haki za binadamu tangu mwaka 2016, ikiituhumu kwamba imekuwa ikiandaa ripoti zisizo na ukweli ambazo zinaonesha kuwa nchi hiyo imekumbwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Burundi imekumbwa na sitofahamu ya kisiasa tangu Aprili 2015 wakati Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza mabadiliko ya katiba yaliyomruhusu yeye kugombea tena awamu ya tatu katika uchaguzi alioshinda mwezi Julai mwaka huo huo.

Kwa mujibu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ambayo Burundi ilijivua uanachama wake, imeeleza kuwa, vurugu zilizotokea nchini humo kati ya Aprili 2015 hadi Mei 2017 zilisababisha vifo vya angalua watu 1,200, huku waliokimbia makazi yao wakikadiriwa kufikia 400,000.

Kumekuwa na hofu kuwa nchi hiyo inatumia nguvu kubwa kujitenga na jumuiya ya kimataifa ili kuepuka kukosolewa pale inapokwenda kinyume na sheria za kimataifa.

Mwezi Novemba Burundi alikataa kushiriki mazungumzo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mabyo yalilenga kutatua mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Juma lililopita taifa hilo liliingia katika mgogoro na Umoja wa Afrika (AU) baada ya kutoa kibali cha kukamatwa kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo,  Pierre Buyoya kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya 1993 ya Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo, Melchior Ndadaye.

Comments

Share.

About Author

Leave A Reply