Tuesday, March 19

Bernard Membe atakiwa kuiga tabia ya Lowassa

0


Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amemtaka aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe kuiga tabia ya Edward Lowassa kwani ni mtu muungwana, na hajawahi kutofautiana au kumsema vibaya Rais wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.

Dkt Bashiru alimmwagia Lowassa sifa hizo na kusema, Waziri Mkuu huyo mstaafu ni mtu muungwana na hana unafiki kwani hajawahi kuzusha wala kutoa kauli mbaya dhidi ya Rais John Magufuli na kumtaka Bernard Membe kuiga tabia hiyo.

Kiongozi huyo wa CCM alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumzia ujumbe uliotumwa kwenye mitandao ya kijamii kwa jina la Barnard Membe aliyekuwa akielezea kutoridhishwa kwake na namna Katibu Mkuu wa CCM alivyomwita ofisini kwake kuthibitisha tuhuma zinazomkabili.

Kauli hiyo ya Dkt Bashiru imekuja wakati mjadala kuhusu madai ya Membe kutaka kugombea Urais mwaka 2020 kupitia CCM yakiendelea kushika kasi, ambapo gazeti moja liliandika kuwa mbunge huyo wa zamani wa Mtama, anakusudia kumkwamisha Rais Dkt Magufuli kugombea Urais kwa awamu ya pili.

Dkt Bashiru alisema kuwa anamheshimu Lowassa kwa uamuzi wake wa kuondoka CCM baada ya kutopewa ridhaa ya kugombea urais na kwenda chama kingine badala ya kubaki ndani ya chama tawala kinafiki na kuwagawa wanachama.

“Mtu kubaki ndani ya CCM kinafiki na kuendelea kugawa chama kwa makundi hatuwezi kumvumilia, na tutahakikisha tunamaliza makundi kwenye chama hicho” aliongeza Dkt Bashiru.

Comments

Share.

About Author

Leave A Reply