Friday, July 19

Aliyoyasema Rostam Aziz baada ya kukutana na Rais Dkt Magufuli Ikulu leo

0


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 13 Novemba, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na wanasiasa Mhe. John Cheyo, Mhe. James Mbatia na Mhe. John Shibuda, na mfanyabiashara Bw. Rostam Aziz Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo hayo Bw. Rostam Aziz amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi bora ambapo amesema anatengeneza misingi imara ya uchumi unaokua kwa uhakika zaidi kwa kujenga miundombinu ikiwemo barabara, reli na bandari ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi na kuzalisha ajira.

Bw. Rostam Aziz amesema anaunga mkono juhudi za Mhe. Rais Magufuli na kubainisha kuwa jukumu la wafanyabiashara ni kutumia fursa nyingi zilizopo katika viwanda, ujenzi na nyinginezo.

“Tunamuunga mkono Rais kwa kuhakikisha Watanzania tunawekeza katika nchi yetu, kukuza uchumi wetu, hilo ndilo la msingi kwa sisi wafanyabiashara” amesema Rostam Aziz.
Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi Mhe. James Mbatia amesema katika kutekeleza malengo 17 ya dunia, Tanzania inafanya vizuri katika lengo la elimu ambalo linazungumzia elimu bora na shirikishi, na amesisitiza kuwa Watanzania wote wana kila sababu ya kuendelea kuijenga nchi yao kwa mawazo ya pamoja yanayozingatia ujumbe uliomo katika wimbo wa Taifa unaosisitiza hekima, umoja na amani.

Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa Mhe. John Shibuda amesema amekutana na Mhe. Rais Magufuli ili kumpongeza kwa uamuzi mzuri alioufanya kutatua tatizo la soko la korosho na kumhakikishia kuwa vyama vya siasa vinamuunga mkono kwa uongozi mzuri unaolenga kurekebisha dosari za mmomonyoko wa maadili ndani ya Serikali na taasisi mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa.

“Katika miaka mitatu, Rais Magufuli amerejesha sifa ya utaifa wetu ya kuwa nchi ya kuaminika na kusadikika na amekweza ari ya uhuru na kujitegemea, tulikuwa na hali duni na dumavu ya maendeleo na ustawi wa jamii, tulikuwa na hali ambayo maendeleo yetu hayawiani na maliasili tulizonazo na rasilimali tulizonazo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha UDP Mhe. John Cheyo amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa msimamo na ujasiri aliouonesha katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake na ametaka Watanzania wajivunie kuwa na Rais ambaye ameonesha dhamira njema ya kufikia nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Sisi Watanzania ni lazima tujivunie Rais tuliyenae, ni Rais anayetoa maamuzi, hata kama yatakuwa magumu kiasi gani, akiamua kusema tunakwenda kujenga Stieglers’ Gorge tutakwenda, akiamua kuwa tunakwenda kujenga standard gauge tunakwenda, akiamua watoto watasoma bure kuanzia darasa la kwanza hadi sekondari inafanyika, na katika miaka mitatu hii imedhihirika kuwa maamuzi yake yanalisaidia Taifa sana” amesema Bw. Cheyo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
13 Novemba, 2018

Comments

Share.

About Author

Leave A Reply