Thursday, February 21

Ajira mpya, kutoongezeka kwa mishahara kunavyokwamisha utekelezaji wa bajeti 2017/18

0


Dodoma: Wakati Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipoanza jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango aliwasilisha bungeni Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti na Mwaka 2019/20.

Wakati akiwasilisha bungeni, Waziri Mpango aliliomba Bunge lipokee, lijadili na kutoa maoni na ushauri kwa ajili ya kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa na kuboresha Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2019/20.

Akizungumza bungeni Waziri Mpango alitaja changamoto mbalimbali ambazo kwa kiwango kikubwa zilizojitokeza katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2017/18 na hivyo kusababisha malengo yaliyokuwa yamewekwa kutofikiwa.

Miongoni mwa mambo yaliyokwamisha utekelezaji huo kwa ufanisi ni ugumu wa kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara waliopo katika sekta isiyo rasmi kwa kuwa hawana sehemu rasmi na za kudumu za kufanyia biashara na hawatunzi kumbukumbu.  Pili ni, kutofikiwa kwa lengo la kodi zinazotokana na ajira (PAYE) kulikosababishwa na kutofikiwa kwa malengo ya ajira mpya na kutoongezeka kwa mishahara kwa wafanyakazi kama ilivyokuwa imetarajiwa.

Vile vile, kodi hizi zimeathirika kutokana na kupunguzwa kazi kwa wafanyakazi kwenye migodi ya madini kufuatia kupungua kwa shughuli za uchimbaji madini kwa baadhi ya migodi.

Tatu ni kushuka kwa biashara za kimataifa kulikopelekea kutofikia malengo ya uingizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi kama ilivyokuwa imetarajiwa. Nne ni upungufu wa wafanyakazi na vitendea kazi ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, hivyo kupunguza ufanisi wa
utendaji kazi wa Mamlaka.

Tano, kupungua kwa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo wakati wa utekelezaji wa bajeti. Changamoto ya sita ni masoko na bei ndogo za mazao kwa wakulima. Saba ni kuendelea kuwepo kwa madai mbalimbali yakiwemo ya wakandarasi, watoa huduma, wazabuni na watumishi wa umma.

Waziri aliongeza kuwa, licha ya changamoto hizo zilizokwamisha utekelezaji wa Mpango wa Bajeti wa 2017/18, serikali imechukua hatua kadhaa kuongeza mapato ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi na utoaji wa elimu kwa walipakodi ili kuongeza mwamko wa kulipa kodi. Pia kuimarisha mifumo na taasisi zinazokusanya mapato ili kudhibiti ukwepaji kodi na uvujaji wa mapato ya Serikali.

Hatua nyingne ni kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara na uwekezaji wa Sekta Binafsi, na kuimarisha ushirikiano na Washirika wa Maendeleo kupitia utekelezaji wa Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo (Development Corporation Framework – DCF).

 

Comments

Share.

About Author

Leave A Reply