Thursday, August 22

WATU 7 WAFA AJALINI KILOLO ,DC ASIA AAGIZA JESHI LA POLISI

0


Baada ya   watu  saba  kupoteza maisha katika ajali ya  gari aina ya  Rav 4  lenye namba za usajili T. 466 AYY Toyota iliyogongana na bajaji  yenye namba za  usajili Mc 104 CAR eneo la  Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo mkoani Iringa  mkuu  wa  wilaya ya Kilolo Asia Abdalah(pichani) aagiza  jeshi la polisi kuchukua hatua kali kwa dereva aliosababisha ajali  hiyo anaripoti mwandishi wetu Francis Godwin kutoka mkoani Iringa

Akizungumza na mwandishi  wa habari  hizi   leo   mkuu  huyo  wa  wilaya  alisema  kuwa  ajali  hiyo  ilitokea siku  ya ijumaa kuu majira ya mchana na  kuwa chanzo cha ajali  hiyo  kinadaiwa ni uzembe wa dereva wa gari kushindwa kulimudu vema  gari lake na  kuhama upande wake na  kuifuata bajaji upande wa  pili.

Mkuu  huyo wa  wilaya ya Kilolo ambae ni mwenyekiti wa kamati ya  ulinzi na usalama   wilaya  hiyo  aliwataja  waliofariki  dunia katika ajali  hiyo  kuwa ni Zena Kikunile ( 8),Sabaha Faraji (35),Musa Ngwembele(58) Yohana Zemela(33),Kondo Chonongwa (20,0)mkazi wa Kijiji cha Mtandika.Tahia Kikunile(12),mkazi wa Kijiji cha Mtandika na Shangwe Kigula(18),mkazi wa Kijiji cha Nyazwa

Alisema  kuwa dereva wa gari  lililosababisha ajali amekamatwa na anashikiliwa na jeshi la polisi hata  hivyo mkuu  huyo wa wilaya alisema ajali hiyo  ni ajali  kubwa ya kwanza  kutokea katika wilaya ya Kilolo na  ofisi yake inalaani vikali tabia za madereva kutozingatia kanuni za barabarani  na kulitaka jeshi la polisi kumchukulia hatua kali dereva huyo na wengine wote wanaokiuka taratibu, kanuni na sheria za barabarani
Pia alisema  katika ajali hiyo watu 5 walipoteza maisha hapo hapo na wawili walipoteza maisha wakiwa hospitali na kufanya jumla ya marehemu 7 kati yao ni watoto wawili na watu wazima 5 akiwemo mama mjamzito na dereva bajaji.

Katika ajali hiyo majeruhi wanne wanaendelea vizuri na mmoja  bado yupo kituo cha Afya Mtandika anaendelea na matibabu hivyo  ametoa pole  kwa  wafiwa  wote  waliopoteza  ndugu zao katika ajali  hiyo na kuwaomba  kuendelea  kuwa  watulivu wakati   wote  kwani  jeshi la polisi  linaendelea na uchunguzi wa  tukio  hilo na kuchukua hatu kwa dereva  aliyesababisha ajali  hiyo.

 kamanda wa  polisi mkoa wa Iringa Juma Bwire baada ya  kutafutwa na mwandishi wa  habari  hizi kwa njia ya simu alisema  yupo  nje ya  ofisi  japo  alithibitisha  kutokea kwa ajali  hiyo na  kuwa taarifa   sahihi ataitoa mara baada ya  kufuatilia zaidi  japo awali taarifa  alizozipata zilikuwa  zikidai ni  watu  watatu ndio  ambao walipoteza maisha .


Share.

About Author

Leave A Reply