Wednesday, August 21

SACH YASAIDIA TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE (JKCI)MASHINE YA KUPIMA JINSI MOYO UNAVYOFANYA KAZI

0


Katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete imepokea mashine ya kupima jinsi moyo unavyofanya kazi “Echocardiography” yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 120 kutoka Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Canada anaripoti Genofeva Matemu – JKCI

Akipokea mashine hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini
ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Willium Mahalu amelishukuru
shirika la SACH Canada kwa kuendelea kuwa wawezeshaji wa taasisi ya SACH Israel
pamoja na kuwaleta madaktari, kuleta vifaa tiba na kutoa mashine ya
Echocardioghraphy kwaajili ya matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo
wanaotibiwa JKCI.

“Tunaishururu taasisi ya SACH kwa kutupatia
mashine ya Echocardiography maana kwa sasa tuna watoto wengi mikoani wanaumwa
magonjwa ya moyo na hawawezi kufika JKCI, hivyo tutaitumia mashine hii
kuwafuata wagonjwa mikoani kutokana na mashine hii kuwa na uwezo wa
kuhamishika” alisema Prof. Mahalu

Aidha Prof. Mahalu alisema kuwa mashine ya Echocardiography
iliyotolewa na SACH imekuja kwa wakati muafaka kwani kwa sasa JKCI imeanzisha
programu za kwenda mikoani kuwafanyia uchunguzi wananchi wasioweza kufika JKCI
hivyo kurahisisha matibabu kwa watoto wenye magonjwa wa moyo waliopo mikoani.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mashine
hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart
– SACH) kutoka nchini Canada Marni Brinder amesema kuwa SACH Canada imedhamiria
kushirikiana na JKCI kutoa huduma bora za matibabu kwa watoto wenye magonjwa ya
moyo Tanzania ili wawe na maisha yenye furaha.

Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa
watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Naiz Majani amesema kuwa
mashine ya Echocardiography ni kifaa muhimu 
katika matibabu ya moyo kwani asilimia 95 za magonjwa ya moyo zinaweza
kutambulika kwa kutumia mashine hiyo, kadhalika hutumika kama kipimo cha awali
kugundua kama mtu ameathirika na magonjwa ya moyo.

Hii ni mara ya sita kwa madaktari kutoka shirika
la SACH kuja hapa nchini kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa watoto wenye
magonjwa ya moyo kwa kushirikiana na madaktari wa JKCI.


Share.

About Author

Leave A Reply