Wednesday, August 21

RAIS DKT MAGUFULI ALIFANYA MAAMUZI MAZURI YA KUTOA VITAMBULISHO KWA WAJASIRIAMALI -DIWANI NGUVU

0


DIWANI  wa  kata ya  Mwangata  katika Manispaa ya  Iringa Edward  Nguvu  Chengula (CCM)  amesema hatua   iliyochukuliwa na Rais Dkt  John Magufuli  ya  utoaji wa vitambulisho  vya wajasiriamali   ni nzuri imelenga  kuwakomboa  wananchi wa kata  yake na  watanzania waliokuwa  wakinyanyasika na  mgambo  wasio  waadilifu .

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi  juu ya   mapokeo ya wananchi wa kata  yake   kuhusu  vitambulisho  hivyo  alisema  kuwa   wananchi  ambao  walikuwa ni  wahitaji  wakubwa wa vitambulisho  hivyo  wameendelea  kujitokeza  kwa  wingi  kuchukua vitambulisho hivyo na  wengi  tayari  wamekuwa na vitambulisho  hivyo .

Chengula  alisema kuwa  kabla ya  kuanza  kwa  zoezi la utoaji wa  vitambulisho   hivyo kata  yake  ilikuwa ni kata ya Kwanza katika mkoa wa Iringa  kuwakusanya  wafanyabiashara  ndogondogo na  kuwakutanisha katika  kongamano maalum la  wajasiliamali hivyo  hata  Rais  alivyokuja na uamuzi wa kutoa  vitambulisho hivyo wananchi  wa kata  yake  walikuwa tayari wamekwisha  pewa mafunzo mbali mbali ya  kujishughulisha katika shughuli mbali mbali .

“Katika  kuonyesha  kuwa  wanaunga  mkono  jitihada  za  Rais Dkt  John Magufuli na serikali ya CCM kwa kazi  nzuri inayoendelea kufanyika  wananchi wangu hawa ambao   wengi  wao  wamekuwa wakifanya kazi za  ujasiriamali  walilazimika  kuchangia hadi huduma  za  kijamii kama  kutoa mifuko ya  saruji kwa  ajili ya uendelezaji  ujenzi wa vyumba vya madarasa  hii ni  kutokana na kumfurahia Rais wetu  kwa kazi nzuri ”  alisema diwani Chengula .

Alisema  pamoja na  wajasiriamali hao kuendelea  kuwa  nguvu  kubwa ya maendeleo ya kata ya Mwangata  bado anaamini  kuwa kwa wale  ambao bado hawajachukua  vitambulisho  vya ujasiriamali na  wanafanya kazi  hiyo  kuchukua  vitambulisho hivyo  ili  kuendelea  kufanya kazi kwa uhuru  zaidi .

Hata   hivyo  aliwataka  wajasiriamali  wa kata  hiyo  kuendelea  kuwapuuza  baadhi ya  wapinzani  ambao  wapo kwa ajili ya  kubeza  shughuli nzuri  za  kimaendeleo zinazoendelea  kufanywa na CCM kwani suala la maendeleo halina itikadi ya  chama .

Katika  hatua  nyingine diwani huyo  alisema  ameendelea  kutatua  kero mbali mbali  ndani ya kata  hiyo ikiwa ni pamoja na kusikiliza  wananchi  wenye  shida na kuendelea  kufanya matengenezo ya miundo mbinu kama barabara ili  kuhakikisha zinapitika wakati  wote na ataendelea  kuwatumikia  wananchi  wake.


Share.

About Author

Leave A Reply