Tuesday, August 20

DC MUFINDI AELEZA KUFURAHISHWA NA R.D.O KUSAIDIA JAMII MAJI

0


Mkuu wa wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Jamhuri wiliam amesema kuwa kazi inayofanywa na shirika lisilo la kiserikali la Rural Development Organization (RDO) ni kubwa na imelenga kuisaidia serikali kutatua changamoto ya maji inayowakabili wananchi Mwandishi wetu Francis Godwin anaripoti kutoka Iringa .

Akizungumza mara baada ya kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa na RDO mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa uongozi wa shirika hilo chini ya mkurugenzi wake Fidelis Filipatali umeendelea kutatua changamoto ya maji kwa wananchi wa kata ya Mdabulo Mufindi ambao awali walikuwa wakisumbuka kutafuta huduma ya maji katika visima na mifereji ya maji ya mito.

” Ninawaomba wananchi wa wilaya ya Mufindi hasa wanaonufaika na mradi huo wa maji kutunza miradi hiyo ya maji na mkumbuke kulipa kama sehemu ya gharama ili kuwezesha kuchangia uendeshaji wa miradi hiyo ya maji isife ” alisema mkuu huyo wa wilaya

kuwa ili miradi hiyo iweze kuwa endelevu na msaada zaidi kwa wananchi kwa miaka mingi mbeleni lazima kuwepo na utunzaji wa miradi hiyo na uchangiaji wa gharama ili kuifanya miradi hiyo kuendelea kuboreshwa zaidi.

Aliwataka viongozi wa serikali ngazi za vitongoji ,vijiiji na kata ambazo zimefikiwa na mradi huo kutunza na kuchukua hatua kali kwa wote watakaofanya hujuma katika miundo mbinu ya maji.

Alisema kuwa azma ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli ni kuendelea kushirikiana na wahisani kama RDO na washiriki wake kuona wananchi wanaendelea kufikiwa na huduma mbali mbali zikiwemo za maji safi na salama .

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa RDO , Filipatali alisema pamoja na kumpongeza mkuu wa wilaya ya Mufindi na uongozi wa serikali ya mkoa wa Iringa katika kutambua kazi kubwa inayofanywa na RDO katika kusaidia kuchangia maendeleo ya mkoa wa Iringa katika utoaji wa huduma ya maji bado alisema wamekuwa wakifanikiwa kutekeleza kazi hiyo kutokana na ufadhili mkubwa ambao umekuwa ukitolewa na wakulima wa Austria na Red Chart .

Filipatali alisema kuwa miradi hiyo ya maji imetekelezwa kata ya Mdabulo vijiji vya Ludilo , Kidete Ikanga na maeneo ya jirani kwa gharama ya zaidi ya Tsh milioni 260 wakati mradi mwingine wa maji ya kutega umetekelezwa kata ya Ihanu vijiji vya ibwanzi, Nandara,Isipii na Lulanda kwa zaidi ya shilingi milioni 210.

Pia Kata ya Luhunga kijiji cha luhunga kimefikiwa na mradi wa maji wa zaidi ya shilingi milioni 160.

Alisema lengo la RDO kuendelea kusaidia wananchi kupatiwa huduma hiyo ya maji na kuwa mbali na wilaya ya Mufindi bado shirika limekuwa likisaidia huduma ya maji wananchi wa wilaya ya Kilolo ndani ya mkoa wa Iringa na kusaidia kutoa elimu ya ufundi kwa watoto wanaotoka familia masikini.

Share.

About Author

Leave A Reply