Tuesday, July 23

MADIWANI WA CCM IRINGA MJINI WASUSA BARAZA LA MADIWANI

0


KIKAO   cha  baraza la madiwani  wa halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa  kimeshindwa  kufanyika  baada ya madiwani wa   chama  cha mapinduzi (CCM)  kususia kikao hicho   wakipinga  kile  walichodai ni ubabe wa mstahiki meya  kupitia  chama  cha Demokrasia na maendeleo  (CHADEMA) Alex  Kimbe katika  uundaji wa kamati mbali mbali na uendeshaji wa vikao hivyo.

Akizunguza leo  na waandishi  wa habari katika   ofisi ya  CCM wilaya ya Iringa mjini naibu meya wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa Joseph Lyata  alisema kuwa  uamuzi wa  kutoingia katika  kikao  hicho   ni kutokana na uamuzi  uliofikiwa na madiwani  wote  wa CCM katika  kikao chao cha  pamoja na  viongozi wa  CCM siku  moja kabla   na kufikia uamuzi wa  kutoshiriki kikao  hicho.

Lyata  alisema  meya  amekuwa  akifanya maamuzi kwa matakwa ya  chama  chake  cha  Chadema na  kuacha  kusimamia  kanuni na taratibu  za  uendeshaji wa  vikao kwa mujibu  wa kanuni halali kanuni   ,kuwa  katika  uundaji wa kamati mbali mbali  madiwani wa  CCM  wamepewa kamati  zisizo na uzito  huku  madiwani wa Chadema  wakipewa kamati  nyeti kama ya  uchumi na fedha ,mipango  miji  na  nyingine  na wa CCM  wakibaguliwa .

” kanuni  zipo  wazi  ili kuweza  kupata wajumbe wa kamati ya  fedha lazima   uchague  majina matatu   ili  kupatikana kwa mjumbe wa kamati hiyo ila  meya  aliteua  jina  mmoja  pekee  la diwani wa  CCM japo hakufanya  vibaya  kumteua diwani wa CCM ila alikiuka  kanuni zinazomtaka  mjumbe  huyo kuchaguliwa na sio kuteuliwa kuingia katika kamati hiyo ”  alisema Lyata

Akitolea  mfano  alisema   kamati ya  UKIMWI mstahiki meya  amempanga  aliyekuwa meya Aman Mwamwindi (CCM) na  mkewe Zainabu  Mwamwindi  jambo  ambalo limewashangaza  na  linaonyesha  hisia  za ubabe  wa meya  huyo .

Alisema  meya  amekuwa akikiuka taratibu  za uendeshaji wa vikao  hivyo kusudi na pale  madiwani wa CCM  wanapopinga  amekuwa akiwapa  adhabu ama  kutowasiiliza  hivyo  wakaona njia pekee ya  kufikisha ujumbe wa  umma na  kuweza kutimiza wajibu wao wa  uwakilishi wa wananchi katika  vikao vya madiwani  kususia kikao  hicho.

Lyata ambae  ndie  alipaswa  kuongoza  kikao  hicho cha baraza la madiwani kutokana na mstahiki meya  kuwa na udhuru  alisema meya  hakumpatia  taarifa  mapema  za  kukaimu nafasi yake na   hivyo asingeweza  kuendesha kikao  pasipo  kuwa na maandalizi  ya kikao  hicho.

Aidha  alisema  wapo tayari  kushiriki  kikao kijacho  kwani  ujumbe  wao kwa  jamii umefika na meya  ameupata kuwa  madiwani wa CCM hawapo tayari  kuendelea  kuburuzwa .

Kwa upande wake  katibu wa madiwani  wa CCM katika  baraza  hilo  Ibarahim Ngwada ambae ni diwani wa Mshindo   alisema  kuwa  wamechoka kuendelea  kuburuzwa na  meya  huyo kwani tayari kupitia nafasi yake  ameweza  kuiingizia hasara kubwa Manispaa kwa  kumpatia  viwanja   zaidi ya 18  mmoja kati ya watu  wake wa  karibu  kinyume na utaratibu .

Pia  wao wanapinga hatua ya  meya  kuruhusu  kibabe  kuvunja  jengo la  kitega uchumi  la Tembo  bar  eneo la  stendi  kuu kwa  kuwa  lilikodishwa  wakati  wa uongozi wa CCM na  hadi leo ujenzi wa  jengo  jipya la ghorofa kama   walivyoahidi  haujafanyika .

Hata   hivyo mstahiki meya wa  Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa Alex Kimbe hakuweza  kupatikana kwa njia ya  simu  ili  kujibu  tuhuma  zilizoelekezwa  kwake  lakini mwenyekiti wa Madiwani  wa Chadema Iringa mjini diwani wa kata ya Mvinjeni Frank  Nyalusi  alisema   walichofanya  CCM ni kuiingiza  Halmashauri katika matumizi mabaya ya   fedha kwani maandalizi ya kikao hicho yametumia pesa za  walipa kodi .

Nyalusi  alisema  upinzani   ndio wamekuwa  wakisusia vikao  bungeni na katika halmashauri kutokana na ukiukwaji wa uendeshaji wa vikao ama  baadhi ya mambo kwenda  kombo  ila  sasa  imekuwa tofauti  baada ya madiwani wa manispaa ya  Iringa kususia kikao .

Aliyekuwa  mstahiki meya  kupitia CCM kipindi kilichopita  Aman Mwamwindi  alisema  kuwa wapo ambao  wanahoji njia   iliyotumika kama ni  sahihi  au  si  sahihi ila wao kama  madiwani wa CCM wameona njia  hiyo ni  sahihi  kwani madiwani wa CCM wote wapo  kwa ajili ya  kutekeleza ilani ya  CCM hivyo jambo la meya wa Chadema  kuwakandamiza madiwani wenye ilani yao ni  kupinga utekelezaji wa ilani jambo ambalo halikubaliki .

“wapo  wanaosema   kuwa  kususa kwetu kikao  tumeiingizia Halmashauri hasara  ya  chakula na posho  ambazo tungepaswa  kupewa  ila  sisi  si madiwani wa  posho ama wa kwenda kula katika  vikao   hivyo ni madiwani wa kupigania maendeleo  wananchi  wetu kama  hoja yao ni posho na chakula inafsi naweza  kuwalisha  chakula na kuwalipa  posho  vikao vijavyo ”  alisema Mwamwindi .

Mwenyekiti  wa CCM wilaya ya  Iringa mjini  Said Rubeya  alisema  kuwa baada ya  kupewa taarifa kutoka kwa naibu meya kuwa madiwani wake  hawajashiriki kikao alilazimika  kuwaita ofisi ya chama na  kufanya nao kikao lakini malalamiko yao  waliyoyatoa  ni ya msingi na chama kimeungana  nao ili  kuona vikao  haviendeshwi kibabe  bali vinaendesha  kwa mujibu wa kanuni na taratibu za  uendeshaji wa  vikao.

Katibu  wa  kikao   hicho mkurugenzi wa Halmashauri ya  Iringa Himid Njovu alisema sababu ya  kutofanyika kwa  kikao hicho ni  kutokana na idadi ya  wajumbe  kuwa pungufu hivyo  kanuni  zinamtaka kuahirisha  baraza kwa  siku saba na kama  wajumbe idadi yao ikiwa ndogo  kanuni zinamruhusu  kuendelea na kikao  cha  baraza la madiwani .

Share.

About Author

Leave A Reply