Thursday, August 22

RAIS MAGUFULI NI KIONA MBALI

0


*WANANGU, WAJUKUU NA VITUKUU VYANGU WATAFAIDI MATUNDA YA JPM*

Ni ngumu sana kwa sasa kumwelewa ama kuelewa nini haswaa anachokifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli (JPM) kwa sasa kutokana na kuwa Rais Magufuli kuwa ni kiona mbali.

Wakubwa wanalalamika safari za nje, semina na posho zimezuiwa; Watumishi wa umma wanalalamika wanabanwa sana kazini kwa sasa; Wapiga dili na Wananchi wanalia pesa hakuna. Malalamiko hayaepukiki kipindi hiki cha mabadiliko makubwa anayoyafanya Rais Magufuli kwa sasa.

Leo hii Rais Magufuli anasisitiza Watu walipe kodi, anavunja mikataba na kuweka makubaliano mazuri kwenye sekta ya madini. Wanangu, Wajukuu na Vitukuu vyangu vitanufaika na matunda ya Taifa letu kupunguza utegemezi na kuweza kujiendesha lenyewe.

Leo hii Rais Magufuli anatumbua majipu, anapandisha kizimbani Mafisadi na wala rushwa. Naiona kesho yetu ambapo tutakuwa na Taifa lenye uadilifu, uaminifu, Taifa linalokemea rushwa na ufisadi kwa vitendo. Nawaona Wanangu, Wajukuu na Vitukuu wakiishi kwenye Taifa safi lisilo na harufu ya rushwa, ufisadi, lenye Watumishi wa umma wenye uadilifu na uwajibikaji wa hali ya juu.

Leo hii Rais Magufuli anazuia mpaka mchanga wa madini uliokuwa unasafirishwa kwenda nje ya nchi. Naiona kesho yetu ambapo kiwanda cha uchekechuaji wa madini, tunaona Watanzania wakipata haki yao stahiki ya madini. Hakika nakiona kizazi changu kikinufaika na rasilimali za Taifa

Rais Magufuli anatumia pesa nyingi kujenga miundo mbinu ya barabara, madaraja, vivuko na barabara za juu. Kesho kizazi changu kitashuhudia Tanzania iliyojengeka yenye mtandao mpana na ulioungika wa barabara, foleni zikiwa ni historia kwao. Naona jamii yangu ikinufaika na uvumilifu wangu wa sasa.

Naendelea kusisitiza anachokifanya Rais Magufuli kwa sasa kitaacha alama isiyofutika kwa Taifa kutokana na kuwa na vitu vinavyoshikika na vyenye mashiko.

Leo hii Rais Magufuli anatumia pesa nyingi kununua ndege, anatumia pesa nyingi sana kujenga reli ya kisasa ya umeme kwa kiwango cha standard gauge. Wapo baadhi yao hawaoni umuhimu.

Mathalani kwenye ujenzi wa reli ya kisasa unaoanzia Dar mpaka Mwanza ambapo kwa hatua ya sasa ujenzi utafikia mpaka Dodoma, baadae kizazi changu kitaona mikoa mbalimbali ikizidi kufunguka kutokana na uwepesi wa usafiri wa haraka kutoka mkoa mmoja hadi mwingine.

Wanangu, Wajukuu na Vitukuu vyangu vitashuhudia Watu, mizigo na mali zao zikisafirishwa kwa haraka mno kutoka eneo moja kwenda eneo lingine, kutoka mkoa mmoja hadi mwingine. Hayo ndio matunda ya uvumilivu na ufungaji mkanda unaofanyika kwa sasa.

Narudia tena kusisitiza, kitendo cha Rais Magufuli kupeleka pesa nyingi sana kwenye miradi ya kimaendeleo tutashuhudia akiandika historia isiyofutika kwa Taifa. Ndege, reli ni baadhi tu ya vitu vya kihistoria ambavyo vizazi na vizazi vitanufaika matunda yake kutokana na mbegu inayopandwa sasa na Rais Magufuli. 

Tutashuhudia mapato yakiongezeka, mzunguko wa pesa ukiwa mkubwa na uchumi wa Watu na wa Taifa ukikua kwa kasi. Yatupasa tuwe wastahimilifu kwa maslahi mapana yetu, ya vizazi na vizazi vyetu.

*Mungu Ibariki Tanzania*
*Na Emmanuel J. Shilatu*Read More

Share.

About Author

Comments are closed.