Thursday, August 22

Wahitimu wasio na uzoefu wa kazi kufaidika na programu ya ajira Serikalini

0


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama. Picha|Mtandao.


  • Serikali imesema inatekeleza programu ya kuwaandaa wahitimu wa vyuo kupata uzoefu wa kazi kabla ya kuajiriwa.
  • Programu hiyo inasaidia kutatua tatizo la ajira katika sekta binafsi.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amesema ofisi yake  imeanza kutekeleza mwongozo mpya wa programu ya kuwaandaa wahitimu wa vyuo kupata uzoefu wa kazi unaohitajika katika soko la ajira. 

Mhagama alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Aida Kenan aliyetaka kujua Serikali haioni kama ni wakati muafaka kuwa na mkakati wa ziada wa programu maalum ya kuwaandaa vijana kabla ya kwenda kazini.

Kenan amesema wahitimu wengi wanakabiliwa na vikwazo mbalimbali wanapoomba kazi na kikwazo namba moja ni kuwa na uzoefu, jambo ambalo ni gumu kwa sababu wanakua wametoka chuoni.

“Ofisi ya Waziri Mkuu inasimamia masuala ya ustawi wa vijana na baada ya kugundua vijana wengi wamekosa fursa za kuajiriwa kwa sababu ya kigezo cha uzoefu. 

“Ofisi ya Waziri Mkuu iliamua kutengeneza mwongozo mpya wa internship (programu ya mafunzo) ili kuhakikisha vijana wanapomaliza masomo yao waweze kupata maeneo ya kupata uzoefu katika private sector (sekta binafsi),” amesema Mhagama. 

Amesema ni kweli  vijana wa Kitanzania wamekuwa wakipata shida kwa kigezo cha uzoefu katika kutafuta ajira na imekuwa ni tatizo ambalo linahitaji ufumbuzi wa kudumu. 


Amebainisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu tayari imeanza kutekeleza mwongozo huo kwa baadhi ya makundi ya vijana ili kuwaandaa kuajiriwa katika maeneo mbalimbali

“Naomba nilihakikishie Bunge lako tukufu kuwa programu hiyo imekwisha kuanza na Ofisi ya Waziri Mkuu imeshasimamia makundi ya kutosha ya vijana kuwapeleka katika maeneo mbalimbali kwa ajili “internship program” tayari kuwafanya wawe na uzoefu wa kuajiriwa,” amesema Mhagama.

Hata hivyo, Waziri huyo hajataja idadi kamili ya vijana waliofaidika na fursa hiyo ya kuandaliwa kuingia katika ajira. 

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Mary Mwanjelwa amesema wameanzisha sera ya ndani ambayo inatoa mwongozo wa ajira katika sekta binafsi. 

“Katika sera yetu mpya ya Utumishi ya 2004, Serikali imesema kabisa kwamba ajira mpya hazitazingatia uzoefu. Uzoefu unakuja kwa wale ambao wako kazini,” amesema Dk Mwanjelwa.

Share.

About Author

Leave A Reply