Thursday, February 21

VYAMA 14 VYAJITOKEZA KUGOMBEA UDIWANI, UBUNGE

0


SUBIRA KASWAGA – AFISA HABARI NEC

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa jumla ya wagombea 13 
walichukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Ubunge katika Majimbo ya
Babati Mjini, Ukerewe, Simanjiro na Serengeti. Akizungumza  ofisini kwake
jijini Dar es Salaam, kuhusu uteuzi huo Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Giveness
Aswile amesema kuwa,  wagombea  hao wanatoka katika vyama sita vya
siasa ambavyo ni AFP, CCM, CUF, NCCR Mageuzi, NRA na UDP.Amesema kuwa, hadi
muda wa mwisho wa uteuzi Novemba 02, mwaka huu saa 10:00 jioni, jumla ya
wagombea wane wa Ubunge kutoka CCM, waliteuliwa na hivyo kutangazwa kuwa
wamepita bila kupingwa kwa mujibu wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Taifa ya
Uchaguzi.Wagombea hao walitangazwa kupita bila kupinga baada ya wanachama
wengine kutoka vyama vilivyochukua fomu za uteuzi, kukosa sifa kutokana na
sababu mbalimbali zikiwemo kushindwa kurudisha fomu hizo kwa wakati na wengine
kutojaza fomu hizo kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutojaza fomu ya kuheshimu na kuyazingatia
maaadili ya uchaguzi. Aidha kwa upande wa udiwani katika kata 47 za Tanzania
Bara, Aswile ameeleza kuwa, vyama 14 vya siasa vilishiriki ambapo wanachama 102
kutoka vyama hicvyo walichukua fomu za uteuzi. “Vyama vilivyoshiriki ni AAFP,
ACT – WAZALENDO, ADC, CCK, CCM, CHADEMA, CUF, DEMOKRASIA MAKINI, NCCR –
Mageuzi, NRA, SAU, TLP, UDP na UPDP” alisema Aswile na kufafanua kuwa, Hadi
Novemba 03, 2018 saa 10:00 jioni wanachama 73 tu ndio waliorejesha fomu na
kuteuliwa kuwa wagombea Udiwani.

Wanachama wengine 29 hawakuteuliwa kuwa
wagombea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kushindwa kurejesha fomu za
uteuzi, kutojaza fomu za uteuzi kwa usahihi, kutosaini fomu za kuheshimu na
kuzingatia maadili ya uchaguzi na kukosa sifa za kugombea udiwani kwa mujibu wa
sheria. Aidha, Aswile amefafanua kuwa wagombea 15 wa nafasi ya Udiwani
waliwekewa pingamizi kwa Msimamizi wa Uchaguzi na kupelekea wagombea 9
kuenguliwa kutoka katika orodha ya wagombea wa nafasi ya udiwani. Tume ya Taifa
ya Uchaguzi ilipokea rufaa mbili kutoka kwa Wagombea Udiwani wa Kata ya Muhinda
iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe na Kata ya Mnyamani iliyopo katika
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala wakipinga maamuzi ya Wasimamizi wa Uchaguzi
kuwaondoa katika kugombea udiwani. Aidha, katika kikao cha Tume kilichofanyika
Novemba 09, 2018 kimeridhia rufaa moja ya mgombea Udiwani wa CUF katika kata ya
Muhinda Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe na hivyo kumrudisha mgombea katika
nafasi hiyo. “Tume imekubaliana na maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi katika kata
ya Mnyamani Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ya kumuondoa mgombea wa CUF katika
orodha ya wagombea na hivyo mgombea kuendelea kuenguliwa kugombea udiwani”
alisema Aswile. Aidha, katika kata 47 jumla ya wagombea udiwani katika kata 41
wamepita bila kupingwa na hivyo ni kata sita tu ndizo zitakazofanya uchaguzi
Mdogo  tarehe 02, Desemba mwaka huu. Amezitaja kata hizo kuwa ni
Nkoanekoli iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Kivinje/Singino, Mteja,
Somanga, Mitole zote katika Halmashauri ya Kilwa na kata ya Butimba iliyopo
Halmashauri ya wilaya ya Bunda.
Kampeni za uchaguzi zimeanza tarehe 04 Novemba 2018 na zitakamilika tarehe
01 Desemba siku moja kabla ya uchaguzi. Aswile amevikumbusha vyama vya siasa na
wagombea kuheshimu Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka
2015 wakati wote wa kampeni na hata siku ya uchaguzi.

Share.

About Author

Leave A Reply