Sunday, August 25

UHARIRI NDIO IDARA MAMA KATIKA KAMPUNI YA UCHAPISHAJI

0


Mwandishi , Hashim Juma
IKS UDSM
Gmail,  Hashimjuma255@gmail.com

Makala  hili tumeigawa katika sehemu kuu tatu, sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo tumefasili dhana mbalimbali zilizojitokeza katika mada sehemu ya pili ni kiini  ambapo tutabainisha umihimu wa idara ya uhariri katika kampuni ya uchapishaji , na mwisho ni hitimisho.

TUKI (2013), wanadai kuwa uhariri ni kazi ya kusoma, kusahihisha na kusanifu miswada ya makala, vitabu na kadhalika. Fasili hii inaelekea kufanana na BAKIZA 2010), juu ya uhariri, kuwa ni mtu anayefanya kazi ya kusoma maandishi kwa ajili ya kusahihisha na kuyasanifu.

Wanaendelea kueleza kuwa mhariri ni mdhamini wa kupitisha na kuweka sawa maandishi yote ndani ya kitabu, gazeti au jarida.

Kuhusu uhariri, Butcher (1992), anadai kuwa kuna aina nne za uhariri ambazo ni; uhariri wa kina, huu ni uhariri ambao hujishughulisha na maudhui na mtindo wa mswada.

 Pia uhariri huu hujihusisha na makosa ya kitaarifa. Aidha mhariri wa jumla, huyu hushughulikia masuala yote ya kiuhariri kuanzia kutafuta mswada, kumtafuta mwandishi, kuwasiliana na mwandishi, kutafuta mikataba na kupendekeza mswada uchapishwe au la.

Aidha fasili hii ya Butcher (k.h.j) haitofautiani sana fasili ya Mallya (1993 na Mulokozi 2014) inayodai dai kuwa uhariri wa jumla unahusisha uendeshaji wa jumla wa michakato ya uchapishaji katika kampuni husika kama vile kubuni miradi, kupokea na kutathmini miswada na kuandaa miswada kwa uchapaji na kadhalika.

Aidha uhariri wa matini, huu hujishughulisha na masuala ya kiufundi kama vile lugha, makosa ya kiuandishi, mpangilio wa matini, vichwa vya habari. Na mwisho ni uhariri wa kuangalia ushikamani wa matini huu ni uhariri unaojikita zaidi kuangalia ushikamani uliopo kwenye maneno yaliopo kwenye mswada.
Wataalamu mbalimbali wanakubaliana kuwa uhariri ndiyo idara mama katika kampuni ya uchapishaji akihusiana na wengine (Mbenna 1983, Kobia 2006, Mulokozi 2014). COPE (2011),   inaeleza kuwa mhariri ndiye anayehusika na kila kitu katika uchapishaji .

Huyu ndiye anayetakiwa kuhakikisha kuwa mswada unachapishwa na kuwa kitabu ikiwa na ubora unaohitajika. Inazidi kueleza kuwa, mhariri ndiye mwenye mahusiano na mwandishi na ndiye anayetakiwa kurudisha mrejesho kwa mwandishi hatua kwa hatua kuhusiana na mswada wake. Yafuatayo ni majukumu ya mhariri katika kampuni ya uchapishaji.

Mhariri huboresha matumizi ya lugha. Mlambo (2007), anasema kuwa mhariri wa matini anathaminika kwa lugha. Mhariri mwenye ujuzi mkubwa wa lugha huwa na uwezo mkubwa wa kuwasilisha mawazo.

Huu ndiyo mswada mkubwa sana kwa waandishi wengi. Mhariri ni mtu makini sana katika kuona na kugundua kosa na kuwa na uwezo na kulisahihisha. Lever akinukuliwa na Mlambo (k.h.j), anasema kutokana na uzoefu wake wa uhariri, mhariri anapaswa kuwa na jicho kali kugundua na kusahihisha makosa ili kukifanya kitabu kiwe bora.

Aidha mhariri anajukumu la kupendekeza aina ya vielelezo vinavyohitajika katika kitabu na kutathmini ufaafu wake. Mlambo (k.h.j), anasema hii hufanyika kwa kushirikiana na mwandishi na msanifu anayeandaa picha, michoro na vielelezo.

 Pia humweleza msanifu wa kitabu kuhusu namna anavyotaka sura ya kitabu ionekane. Hapa ndipo mhariri huonekana kuwa kiungo kati ya mwandishi na msanifu. Aidha mhariri ndiye hutoa maagizo kwa mtoaji wa kitabu na mpigachapa, akiwamo mpangaji herufi.

Mhariri anajukumu la kuyapima maudhui ya mswada kama yanafaa au la. Hapa mhariri huwa na jukumu la msingi la kushughulikia maudhui ya mwandishi kwa kuangalia kama yamewasilishwa vema na yamezingatia maadili na mtazamo wa kampuni yake. Mhariri huamua maudhui ya kitabu kwa kuzingatia mchango wa washiriki wengine (taz Feather 2003, Mlambo 2007) wanaeleza kuwa mhariri akishaangalia maudhui na kuyaelewa ndipo anapoweza kuwa na sababu ya kumshawishi mwandishi kuhusu kuondoa au kuongeza jambo katika mswada wake.

Mhariri anajukumu la kufanya kazi kwa ukaribu sana na mwandishi ili kuboresha mswada, Kwa miswada ya kibunifu hufanya hivyo ili kazi iwe na mpangilio mzuri wa visa, namna nzuri ya uwasilishaji na mawazo, ujengaji wa wahusika, mandhari na mtiririko pale panapohitajika au kulazimu (taz Montages, gross) wanakubalina kuwa mhariri hana budi kutambua kuwa maandishi ni ya mwandishi na lazima yaheshimiwe na kubaki kama yalivyokuwa.

Mhariri anajukumu la kulinda sauti ya mwandishi katika mswada. Pacho (2017), anadai kuwa mhariri hapaswi kuandika upya kitabu au kubadili maudhui na sauti ya mwandishi, kwani yeye ni kama kiongozi na mkunga ambaye anapaswa kuchukua jukumu la kulea mtoto mpya anayezaliwa.

 Mhariri mzuri ni yule ambaye hataki mawazo yake yatawale kitab una kumfanya yeye kuwa kama mwandishi mwenza. Mhariri anapaswa kutambua dhahabu iliyomo katika mswada wa mwandishi na kutafuta namna ya kuichimba dhahabu hiyo na kuiweka katika namna ambayo itainufaisha jamii nzima zaidi ya kampuni pekee.

Mhariri anajukumu la kuangalia muunganiko wa visa. Pacho (k.h.j), anadai kuwa ia mhariri huhakikisha kuwa kuna msuko na mtiririko sahihi wa visa katika hadithi.

Hapa mhariri atalazimika kusoma hadithi yote kuona kama visa vinaoana na kuchukuana, kuangalia kama kuna mapengo au baadhi ya visa vinaning’inia. Kadhalika, anapaswa kuangalia kama wahusika wake wanajitosheleza na wanajibainisha baina yao na wanaongea kwa sauti zao wenyewe  na kuonesha tabia zao.

 Pia huangalia mpangilio wa aya na sentensi kama kuna aya ndefu sana zinapaswa kutengwa katika aya fupifupi.

Aidha mhariri anajukumu la masuala ya haki za kisheria. Greco (k.h.j), anaeleza kuwa mhariri ni kama mlinzi wa langoni ambaye huwa na mustakabali wa mswada na kampuni yake, kuamua ni jambo gani zuri na la muhimu liwemo na lipi lisiwemo. Aidha Butcher (k.h.j), anaeleza kuwa mhariri lazima ajiulize ni kazi yake kweli au kaiba kwa wengine na kuifanya yake.

Hili ndilo jukumu la msingi kama unataka kunusuru kampuni yako na migogoro na waandishi na makampuni mengine kwa kurudia kazi zao bila ruhusa yao.

                                                                 MAREJELEO
BAKIZA, (2010). Kamusi la Kiswahili Fasaha. Nairobi: OUP.
Butcher, J (1992). Copy-Editing: The Cambridge Handbook: New York. Cambridge University           Press.
COPE, “A short Guide to Ethical Editing for New Editors” Publicationerethics.org/files/short-
                  guide-to-ethical-editing-for-new-editors.pdf. 2019/04/18.
Feather, J. (2003). Communicating Knowledge: Publishing in the 21st Century. Chippenham:          Antony Rowe ltd.
Greco, A.N. (2005). The Book Publishing Industry. Mahwah: Lawrance Erlbaum Associates.
Kobia, M.J (2006). “Uchapishaji wa FasihiSimulizi nchini Kenya: Mtazamo Changamoto na          Mustakabali wake” katika Kiswahili. Juz,69. Dar es Salaam: TUKI kur 93-108.
Mulokozi, M. M (2014). Utangulizi a Uchapishaji kwa Kiswahili. “Idara ya Fasihi
                      na Uchapishaji, TATAKI. (Haijachapishwa).
Mallya, J. M. K (1993). Uandishi na Matatizo ya Uchapishaji Tanzania, “Katika Makala ya semina         ya umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania, Fasihi, Uandishi na Uchapishaji.

  Mulokozi, M.M na C.G Mungongo. (wah). Dar es Salaam.

Mbenna, C.I (1983). “Namna ya kuandaa Miswada ya Vitabu,” katika Makala za Semina ya         kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili II, Uandishi na Uchapishaji. Dar es Salaam:         TUKI.
Mlambo, A. (2007). African Scholary Publishing Essays. Oxford: African Books Collective Ltd.

Pacho, P. J. (2017). Athari ya Mhariri Katika Mswada. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
                      Tasnifu ya umahiri  (Haijachapishwa).

Share.

About Author

Leave A Reply