Sunday, August 25

TBL yang’ara mauzo soko la Hisa Dar

0


Wakati TBL, CRDB na NICO zikiongoza kwa mauzo ya hisa, kampuni ya Acacia imekuwa kampuni pekee ambayo wawekezaji wake leo watalala wakiwa na furaha baada ya hisa za kampuni hiyo kupanda kwa asilimia 2.19. Picha|Mtandao.

  • Yaongoza kwa kuuza kiwango kikubwa cha hisa kikiwa ni asilimia 66.5 ya hisa zote zilizouzwa sokoni leo.
  • Hata hivyo, thamani ya hisa zake imebaki kama ilivyokuwa mwishoni mwa juma lililopita.
  • Wawekezaji wa EABL, JHL watalala na maumivu baada ya thamani ya kampuni hizo kupungua. 

Dar es Salaam. Kampuni ya bia Tanzania (TBL) leo imeng’ara katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) baada ya kuongoza kwa kuuza kiwango kikubwa cha hisa ambacho ni sawa asilimia 66.5 ya hisa zote zilizouzwa sokoni hapo leo. 

Ripoti ya soko ya siku ya DSE ya Mei 27 inaonyesha kuwa TBL imefanikiwa kuuza hisa 26,050 ya hisa kati ya 39,191 zilizouzwa sokoni leo (Mei 27, 2019) ikifuatiwa na benki ya CRDB (7,053) na kampuni ya uwekezaji ya NICO (4,500).

Makampuni hayo matatu ndiyo yaliyofanya vizuri zaidi leo kwa kuuza hisa nyingi sokoni. 

Licha ya TBL kuongoza kuuza kiwango kikubwa, thamani ya hisa zake hazijapanda imebaki kama ilivyokuwa ijumaa ya Mei 24, 2019 ambapo hisa moja imeuzwa kwa Sh11,400.


Wakati TBL, CRDB na NICO zikiongoza kwa mauzo ya hisa, kampuni ya Acacia imekuwa kampuni pekee ambayo wawekezaji wake leo watalala wakiwa na furaha baada ya hisa za kampuni hiyo kupanda kwa asilimia 2.19. 

Wawekezaji hao wamepata Sh100 zaidi kwa kila hisa moja kutoka kiwango cha ijumaa Mei 24, 2019 ambapo ripoti ya leo ya DSE inaonyesha kuwa hadi soko linafungwa thamani ya hisa moja ya Acacia ilikuwa ni Sh4,660 kutoka Sh4,560 iliyorekodiwa ijumaa. 

Hata hivyo, ripoti hiyo inaonyesha kuwa thamani ya hisa za kampuni ya  bia ya East African Breweries Ltd (EABL) imeshuka kwa asilimia 0.43 na kampuni ya hodhi ya Jubilee (JHL) imeshuka kwa asilimia 1.09.

JHL ndiyo kampuni iliyofanya vibaya zaidi leo sokoni huku nyingi zikibaki katika viwango vilivyokuwepo jana zikiwemo Vodacom, na benki ya NMB, Swala na Swis. 

Share.

About Author

Leave A Reply