Sunday, August 25

Taasisi 40 za Serikali zenye mapungufu makubwa katika Tehama zatajwa

0


  • Zipo wizara, idara na balozi ambapo hazina utaratibu au sera zinazotoa uhakika kuwa teknolojia ya habari na mawasiliano inayotumiwa na taasisi inafanya kazi kama inavyotarajiwa.
  • Idadi ya taasisi hizo imeongezeka kutoka 31 mwaka 2016/2017 hadi 40 mwaka 2017/2018. 
  • Hali hiyo inaziweka taasisi hizo katika hatari ya kupata majanga.

Dar es Salaam. Taasisi 40 zikiwemo wizara na idara za Serikali zimebainika kuwa na mapungufu makubwa ya kutokua na sera, mpango mkakati wa kuendeleza teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), jambo linaloziweka katika hatari ya kupata majanga ya mifumo ya kidijitali.  

Udhibiti wa Tehama ni utaratibu au sera ambazo hutoa uhakika kwamba teknolojia ya habari inayotumiwa na taasisi inafanya kazi kama inavyotarajiwa; na kuwa, data ni za uhakika na taasisi inafuata sheria na kanuni zilizopo katika tathmini ya tehama.

Mapungufu hayo yamebainika katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kuhusu hesabu za Serikali Kuu ya mwaka 2017/2018 ambapo matokeo ya ukaguzi yalionesha kuwa katika sampuli ya taasisi 40 zilizopatikana na mapungufu makubwa ya Tehama ni wizara 10, sekretarieti ya mikoa (11), mawakala (8), taasisi nyingine (6) na balozi  tano.

Baadhi ya mapungufu hayo ni kutokuandaa mpango na sera wa teknolojia ya habari na vifaa vya kuzuia majanga.

“Ukosefu wa mifumo ya habari ya upatikanaji wa kudhibiti unaweza kusababisha hatari ya kuwa na watumiaji ambao hawana ruhusa kupata mifumo ambayo inaweza kuathiri usiri wa mfumo, uaminifu na upatikanaji wa mifumo ya Tehama,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo. 


Hata hivyo, idadi ya taasisi hizo zenye mapungufu katika Tehama imeongezeka kutoka 31 mwaka 2016/2017 hadi 40 ikiwa ni ongezeko la asilimia 29 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. 

CAG ametoa mapendekeza kwa Maafisa Masuuli wa taasisi husika kuhakikisha kuwa mfumo una usimamizi sahihi na Serikali inapaswa kuwa na muundo mzuri wa mipango ya kukabiliana na majanga na mikakati ya kuhakikisha kuwa vifaa vya kompyuta na programu vinatunzwa ili kuweza kukabiliana na majanga pale yanapotokea. 


Ripoti ya utafiti wa Ushindani Duniani (‘Global Competitiveness Index 2018’)  imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 za mwisho duniani kwa kasi ndogo ya matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) jambo linalofanya ishindwe kutumia ipasavyo fursa zitokanazo na sekta hiyo katika kuleta maendeleo.

Ripoti hiyo ilitolewa Oktoba 2018 na Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum) ambapo imeiweka Tanzania katika nafasi ya 135 katika ya nchi 140 zilizofanyiwa utafiti huo. Mwaka 2017, Tanzania ilishika nafasi 122 kati ya nchi 137 zilizofanyiwa utafiti.

Ripoti hiyo inadai kuwa licha ya kuwepo kwa vyanzo mbalimbali vya upatikanaji wa mtandao bado kasi ya intaneti inayotumiwa na taasisi na mashirika (Fixed-broadband Internet subscriptions ) kwajili ya shughuli za kiofisi ni ndogo. 

Share.

About Author

Leave A Reply