Thursday, August 22

Silaha za ushindi zinazoweza kuwasaidia wanafunzi kidato cha sita 2019

0


  • Mwanafunzi ajiandae kiisaikolojia kwa kujenga fikra za kujiamini na kuhakikisha afya ya akili na mwili iko sawa kuukabili mtihani. 
  • Walimu wana wajibu wa kuwaandaa vema wanafunzi kwa kuwafundisha mbinu za kufaulu mtihani.
  • Tathmini ya muda uliobaki kabla ya kufanya mtihani ifanyike ili kutoa kipaumbele kusoma notsi chache na masomo unayoyaelewa zaidi. 

Dar es Salaam. Kufeli sio jambo la kufurahisha kwa mtu yeyote iwe kimasomo au maisha. Hata kwa wanafunzi waliopo shuleni ambao wanategemea kutimiza ndoto zao kuelimika na kupata taaluma watakazozitumia kuendeleza maisha, kufeli ni moja ya masuala hawaombei wakumbane nayo. 

Lakini kufeli kunaweza kuepukwa ikiwa mwanafunzi amejiandaa vizuri kuukabili mtihani. Kufaulu mtihani kunategemea pia mbinu mbalimbali ambazo zikitumika vizuri zinaweza kumtoa mwanafunzi kimasomo.

Wadau wa elimu wakiwemo wanasaikolojia na wahadhiri wa vyuo vikuu wameweka wazi mbinu wanazoweza kutumia watahiniwa wa kidato cha sita ambao wanatarajia kutupa karata yao ya mwisho katika mitihani ya Taifa Mei mwaka huu. 

Mbinu hizo hizo ni pamoja na saikolojia ya mwanafunzi anayetarajia kufanya mtihani kuwa sawa ikiwemo afya njema ya akili na mwili ambayo ina mchango mkubwa kwa mwanafunzi kufanya vizuri.

Ishinde hofu ya kufeli mtihani

Mtaalam wa Saikolojia kutoka kampuni ya DM Saikolojia Limited,  Dosi Said Dosi anasema maandalizi ya mwanafunzi kuelekea kwenye mtihani yanaanza kwa kuepuka mawazo hasi yanayoambatana na hofu ya kufeli mtihani hata kabla hujafanya. 

“Hofu ya mtihani ni ile hali ambapo mtu anakua na uwoga uliopitiliza kukabiliana na mitihani inayotarajiwa kuifanya. Hofu hii huathiri saikolojia ya mtu katika pande zote za kiakili, kijamii, kihisia na kimwili,” anasema Dosi.

Katika kukabiliana na hofu ya mtihani ambayo husababishwa na kutojiamini, ukubwa wa mtihani, historia ya kufeli kipindi cha nyuma na kusemwa vibaya na wazazi, anasema mwanafunzi anatakiwa kusoma vizuri na kwa upana masomo yote ambayo unaenda kuyafanyia mitihani huku akijiamini kuwa ameshinda tayari. 

Pia mwanafunzi anatakiwa kuweka matini yake katika mpangilio mzuri ili kusaidia kuweza kukumbuka kwa urahisi na kumpunguzia hofu.

“Achana na mawazo hasi, jiamini una uwezo wa kufanya vizuri na kubadili matokeo. Wapo watu ambao walifeli kwenye mitihani ya moko na wakaja wakafaulu mitihani ya Taifa. Hivyo amini hata wewe unaweza,” anasisitiza Dosi.

Jiamini, jione ni mshindi. Ondoa hofu ya mtihani, mafanikio ni ya kwako. Picha| Mtandao.

Kula, lala na pumzika kwa wakati

Wakati huu wanafunzi hutumia muda mwingi kusoma na kusahau kula na hata kupumzika wakihofia mtihani. 

Mwanasaikolojia Dosi anasema pumzisha mwili na akili kabla ya kwenda kwenye mitihani ili mwili na akili viwe katika hali nzuri ya kukabiliana na mitihani.

Mtihani ni pamoja na kujali afya ya mwili wako, chukua tahadhari ya kujilinda dhidi ya maradhi nyemelezi kwa kula vizuri na kujua hali ya afya yako kama inaruhusu kufanya mtihani. 

“Ni vizuri wanafunzi wakajua afya zao mapema kabla ya siku ya mtihani. Kama wana dalili za malaria au magonjwa mengine basi watibiwe mapema,” anasema Mhadhiri wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Lugome.

Wanafunzi, walimu au wazazi wanashauriwa kutokupuuzia dalili za ugonjwa wa wanafunzi wanapokaribia mitihani kwa kudhani kuwa watawapotezea muda wa kujiandaa na mitihani.

Kula, lala na pumzika kwa wakati ili kuipa nafasi akili kufikiri vizuri. Picha|Mtandao.

Wajibu wa walimu kwa watahiniwa

Wakati Dosi akisisitiza wanafunzi kuishinda hofu ya mtihani, Lugome anasema walimu wawakumbushe wanafunzi kutojiamini kupita kiasi wasichukulie mtihani kama kitu cha kawaida kwa kupuuzia kujiandaa na matokeo ya mtihani yakitoka wanalalamika kuonewa. 

Katika muda uliobaki, wanafunzi wafundishwe jinsi ya kujibu mtihani kwa ufasaha. Hili linawezekana kama watapewa mitihani ya miaka iliyopita na kusoma katika makundi ili kubadilishana mawazo na uzoefu.

“Ni vema wanafunzi wakafundishwa mbinu sahihi za kujibu maswali kwenye mtihani na ikiwezekana wapewe mazoezi ya kutosha ili wazoee mbinu hizo. Mtihani bila maandalizi ni sawa na timu kwenda kwenye mashindano bila ya mazoezi ya kutosha,” anasisitiza Lugome ambaye amekuwa akisisimamia mitihani vyuo vikuu.

Wakati huu wa lala salama, sio vizuri kujifunza maarifa mapya au mwalimu kuanzisha mada ngumu na mpya kipindi cha kukaribia mitihani. Jambo hilo linaweza kuwavuruga wanafunzi na watashindwa kujiandaa vema. 

Lugome anasema ikitokea hadi siku chache kabla ya mitihani kuna mada mpya haijafundishwa hata kama ipo kwenye muhtasari wa somo basi hakuna sababu kufundisha mada hiyo kwani kwa kufanya hivyo utawachanganya wanafunzi na kuwaathiri kisaikolojia.

Tathmini na fahamu muda uliosalia kabla ya kufanya mtihani

Mtaalam wa teknolojia ya usimamizi wa taarifa za rasilimali watu katika sekta ya elimu, Kanungila Karim anasema kufanya tathmini ya muda ni njia rahisi inayoweza kukufanya ufaulu mtihani tena ukiwa na uhakika.

Tathimini ni kipimo sahihi kitakachokufanya ujue upungufu wako uko wapi na nini ufanye kulingana na muda ambao utakuwa umesalia kabla ya kufanya mtihani.

Kama muda umebaki mchache na mambo ni mengi, basi soma notsi fupi zilizoandaliwa vizuri kuliko kupoteza muda kwa kusoma mambo ambayo unajua huwezi kumaliza kwa wakati. 

“Njia hii itakusaidia kutokuishiwa hamu ya kusoma. Notsi fupi husaidia kuelewa haraka na kwa mujibu wa wataalamu wanadai notsi hiyo husaidia sana kumtunzia mwanafunzi kumbumbu nzuri,” anasema Karim.

Mfano wa notsi fupi na nzuri ni zile zinazotolewa na programu tumishi (App) ya  “Thl Tanzania” kwenye vifaa vya elektroniki vya simu, tableti na kompyuta mpakato.

Sambamba na hilo, Karim anasema wanafunzi watumie muda mwingi kusoma masomo unayoyaelewa vizuri. Haimaanishi uache kusoma masomo mengine, ila yape kipaumbele masomo ambayo unajua yatakubeba katika matokeo ya mtihani  alama za masomo tofauti tofauti na siyo somo moja tu.

Aidha mtandao huu unawatakia mafanikio katika mitihani yenu

Share.

About Author

Leave A Reply