Monday, June 17

SERIKALI YATOA SIKU 4 KWA WANUNUZI WA KOROSHO VINGINEVYO………

0Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa tamko leo Nov 9, 2018

*Yawataka waandike barua wakionesha tani wanazohitaji na lini
watazichukua

*Yasema zaidi ya hapo haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho
tena

NA OWM, DODOMA

SERIKALI
imetoa siku nne kwa wanunuzi wote 35 waliojiandikisha kununua korosho wawe
wamepeleka barua katika Ofisi ya Waziri Mkuu wakionesha  kiasi cha
tani wanazohitaji na lini watazichukua.

“Hivyo
wanunuzi waliojiandikisha wakiwemo na wale wote ambao wamekuwa wananunua kwenye
minada lakini kwa kiasi kidogo, wahakikishe ndani ya siku hizo nne kuanzia leo
Ijumaa hadi Jumatatu saa 10 alasiri wawe wameleta barua na ofisi yangu ipo wazi
saa 24.”

Hayo
yamesemwa leo (Ijumaa, Novemba 9, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati
akitoa tamko la Serikali kuhusu ununuzi wa zao la korosho, ofisini kwake
Mlimwa, jijini Dodoma.

Baada
ya kupita siku hizo Serikali italazimika kufuta usajili kwa wote waliojisajili
kununua zao hilo kwa sababu walikubaliana kwenda kununua lakini hali
inayoonekana sasa ni kama kumkomoa mkulima kitu ambacho imesema haitakubaliana
nacho.

“Mwenye
nia ahakikishe katika siku hizo nne iwe ndio mwisho wa kununua korosho na
waandike barua kwani ofisi yangu ipo wazi saa 24 wana nafasi ya kuleta barua
wakati wowote wakionesha nia yao na kiwango wanachokihitaji. Zaidi ya hapo
Serikali haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena.”

Waziri
Mkuu amesema kwenye msimu wa ununuzi wa korosho wa mwaka huu, walishuhudia
kusuasua kwa minada, ambapo Serikali ilikutana na wanunuzi wa korosho katika
kikao kilichoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ambapo walikubaliana kununua
kwa bei inayoanzia sh 3,000 na kuendelea.

“Mjadala
ulikuwa wa wazi na wafanyabiashara wenyewe walipendekeza bei ambayo ilikuwa inaanzia
sh. 3,000, hata hivyo baada ya kikao hicho ununuzi katika minada imeendelea
kusuasua na hata tani zilizokuwa zikinunuliwa zilikuwa kidogo sana. Sisi
tunaiona hali hii kama mgomo baridi ambao si sawa sawa sana kwani malengo yetu
sisi na sekta binafsi ni kumfanya mkulima apate bei nzuri.

Hali
hii haifurahishi kwa sababu Serikali imedhamiria kuboresha mazao yanayolimwa na
wakulima kwa kuwasaidia kuanzia katika hatua za utayarishaji wa mashamba,
upatikanaji wa pembejeo na masoko ili waweze kunufaika na kilimo na kupata tija
katika mazao hayo.”

Waziri
Mkuu amesema baada ya kugundua bei imekuwa tatizo Serikali ilifanya jitihada za
kupeleka wataalamu wake katika masoko makuu duniani na kupata bei halisi ambayo
bado  inatosha kumlipa mkulima sh 3,000.

Hatua
hiyo imekuja baada ya zao la korosho kuendelea kununuliwa kwa bei ya chini na
idadi ya wanunuzi kuwa ya chini licha ya uzalishaji wa mwaka huu kuwa mdogo
ukilinganisha na msimu wa mwaka jana.

Amesema
msimu wa mwaka jana uzalishaji ulikuwa zaidi ya tani 300,000 na mwaka huu
zinatarajiwa tani zaidi ya 200,000 hivyo wafanyabiashara wanao uwezo kununua
korosho zilizopo.

Hata
hivyo Serikali imewataka wananchi hususani wakulima wa korosho nchini kuendelea
kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kushughulikia suala hilo.

Share.

About Author

Leave A Reply