Saturday, August 24

MUUNDO WA RIWAYA

0Na mtaalamu wetu

S.A.K. Mlacha 

@MASSHELE

Riwaya ya Kiswahili bado ingali changa sana katika upande wa uchambuzi na uhakiki. Historia ya uhakiki wa riwaya ya Kiswahili ambayo imechukua karibu muda wa miaka ishirini hivi sasa,

 imeonyesha kuwa wataalamu wengi waliofanya uchambuzi wa riwaya ya Kiswahili hawakujaribu kwenda na wakati na kuzitumia njia za kisasa za uchambuzi. Kwa hali hiyo, riwaya ya Kiswahili imebaki nyuma na kuathirika sana kwa upande huo. Wengi wa wahakiki hao wameviangalia vipengele vichache tu kama vipengele huru au mara chache sana wamejaribu kuvihusisha na vipengele vingine kama itakavyojadiliwa hapo baadaye.

Mitindo hii ya kuichambua riwaya ambayo ilizoeleka na kuwa ya kawaida kwa karibu kila mwana-fasihi ilionekana kuwa finyu mno. Hii ilikuwa ni kuiangalia riwaya kwa kutumia dhamira, wahusika, lugha au msuko wa matukio bila kujali uhusiano wao kwa pamoja. Kasoro yake kubwa ilikuwa ni kutoikamilisha riwaya kwa vile wahakiki walijikita kwenye kipengele kimoja kimoja tu. Uchambuzi wa aina hii huiangalia riwaya nusu nusu na kuuacha ushikamano na muambatano wake ambao hasa ndio unaoweza kuonyesha na kutupatia undani wa riwaya hiyo kimaana na vilevile kuonyesha umuhimu wa kila kipengele katika kuijenga kazi nzima. Uchambuzi huu ni sawa na kuangalia umbo la binadamu kwa nje na kuzingatia kila kiungo chake pekee badala ya kukiangalia kiungo hicho katika uhusiano wake wa kutegemeana na kusaidiana na viungo vingine. Uchambuzi sahihi ni ule unaoangalia kila kiungo nje na ndani na jinsi kinavyohusiana na vingine nje na ndani. Njia mojawapo ya kisasa ya kukamilisha uhakiki wa riwaya ya Kiswahili ni kuangalia muundo wake kwa kutumia vipengele vyote na jinsi vinavyohusiana na kutegemeana. Lakini kabla hatujaangalia muundo huo ni muhimu tuangalie kazi zingine za uhakiki na kuona mafanikio na kasoro zake.

Kazi za mwanzo za uhakiki wa riwaya ya Kiswahili ni pamoja na Hisi zetu(1973 na 1974), Ndimi zetu (1974),Uchambuzi wa Maandishi ya Kiswahili(1968), Aggressive Prose (1981). Aidha makala kadhaa ya uhakiki yalijitokeza sana katika majarida ya Mulika naKiswahili. Kazi hizi za nwanzo za uhakiki, na hata zile za baadaye, zilikuwa ni mchango mkubwa sana katika juhudi za kuiendeleza na kuikomaza riwaya ya Kiswahili. Mchango wao zaidi ulikuwa kwenye kujaribu kufafanua riwaya na kuiangalia kwa upana ambao ulikuwa unafaa kwa wakati wa mwanzo, wakati ambapo riwaya ya Kiswahili ilianza kuingizwa kwenye shule na fasihi kuchukuliwa kama somo muhimu mashuleni na hata Chuo Kikuu. Ni wazi kila mwanzo una ugumu wake; na hivyo uhakiki wa mwanzo haukutawaliwa na mabadiliko yoyote ya kitaalamu. Waandishi wa riwaya walizidi kupevuka wakati wahakiki walibakia nyuma na kutumia nyenzo zilezile za zamani. Hali hii iliwaathiri wanafunzi wa fasihi katika shule, na kwa kiasi fulani katika vyuo, kwani wanafunzi hao wangetakiwa wasogezwe mbele katika kuielewa riwaya ya Kiswahili.

Pamoja na hayo yote, kazi hizo za awali bado zilikuwa finyu si kinadharia tu bali hata kwa kiwango cha uchambuzi. Uchambuzi huu, ambao ulikuwa haujakomaa, ulilemewa na kuongozwa na hisia na hemko la kisiasa. Matokeo yake ni kuwa badala ya nadharia kadhaa kujitokeza kazi nyingi za uhakiki zilionekana ni maelezo na mazungumzo ya ziada kuhusu vitabu vilivyojadiliwa. Kazi hizo hazikuonyesha ufundi wa uhakiki wa kuunda au wa kumfunza mwanafunzi aweze kuisoma kazi ya fasihi na kuweza kuiona kwa jicho huru na pia kuunda jibu lililo sahihi kulingana na mategemeo ya mwalimu mhakiki. Wahakiki hawakujiona wasanii na wala hawakuowaona wanafunzi wa fasihi kama wabunifu na mabingwa wa kuona kitu kipya. Walijiona na kuwaona wanafunzi wao kama wafafanuzi wa kile kilichoundwa na mwandishi na ambacho hawawezi kukivunja na kukijenga upya. Kwa hivyo hawakuziangalia kazi nyingi kwa undani unaostahiki. Hii yawezekana ilitokana na hali ya kwamba wahakiki wengi hawakutaka kuzingatia jinsi riwaya ilivyojengwa au miundo iliyojitokeza ambayo kwayo wangeweza kuitafakari riwaya yoyote ile na kuiunda upya kwa kutumia miondoko au mianzo tofauti, iwe kwa kuanza na dhamira, wahusika, lugha, maneno, isimu, taswira au kipengele chochote kile cha lugha, fasihi, elimu jamii na hata fani nyingine kama vile falsafa, saikolojia au siasa.

Wahakiki wa awali, kama vile wahakiki wengine hata hivi leo, walikuwa na lengo la kuifunza jamii namna ya kuisoma riwaya na kutambua dhanura au vile vipengele muhimu vya riwaya. Ingawa wengi wao walizingatia kusifia au kukashifu kazi hizo kwa kutumia maneno kama vile, “kazi hii imefanikiwa sana; mwandishi huyu ameshindwa…” na kadhalika, kwao hadhira yao kubwa ilikuwa kama tulivyogusia awali, wanafunzi wa fasihi ambao ‘walitakiwa’ kujua uzuri na ubaya wa kazi ya fasihi au katika kazi ya fasihi. HaJi hii ilisababisha madhara ya aina mbili muhimu katika uhakiki wa riwaya ya Kiswahili. Kwanza kabisa, kwa vile kiwango cha uhakiki wao kilikuwa kile kinachowastahilia wanafunzi wa sekondari, wakufunzi na wahakiki wanagenzi wa wakati huo, walichelewa sana na hata kushindwa kukivuka kiwango kilichozoeleka. Aidha wanafunzi nao pia walitawaliwa na mawazo ya kiwango hicho hicho. Jambo jingine ni kuwa uhakiki wao, ambao kwa kweli ulitokana na kuiga uhakiki mwepesi na rahisi wa akina Palmer (1972), Wright (1973), Cook (1977) na hata Killam (1980) ambao walitayarisha kazi za aina hiyo katika fasihi ya Afrika kwa Kiingereza. Wahakiki hao wa riwaya ya Kiswahili hawakuwapa fursa wanafunzi wa fasihi kuwa makini na wabunifu katika kuiangalia kazi nzima. Msisitizo uliendelea kuwa kwenye kuifafanua kazi. Kwa hali hiyo basi, kazi zote za uhakiki zimekuwa na muundo wa aina moja kwa kurudia mambo yaliyo dhahiri katika vitabu na sio kuunda jambo jipya linalotokana na kuiangalia liwaya kwa undani zaidi.

Uhakiki wa riwaya sio kuirahisisha riwaya au kufafanua wazo moja na jingine. Uhakiki ni ufundi wa kisanii wa kuiangalia riwaya au kazi yoyote ile na kuweza kuiona katika pande zote, katika undani wake kimaumbile na mwendo na namna zote zinazoifanya kazi hiyo iwe ilivyo. Ni ufundi wa kuangalia jinsi lugha au maneno yalivyotumika kama vile damu katika mwili wa binadamu, kuunganisha kila kipengele kinachoweza kujadiliwa katika riwaya na wakati huo huo riwaya ibaki ikionekana katika hali kamili na bila kupotosha maana. Kwa mfano, wahusika huhusiana sana na kutegemeana na lugha na dhamira. Vyote hivi huhusiana na kutegemeana na mtiririko wa matukio na fani ya mwandishi. Hii ni pamoja na kuwa kila kipengele kina vijipengele vyake ambavyo vinakikamilisha. Katika lugha kuna vipengele muhimu kama vile uundaji wa maneno, semi, methali, isimu jamii, uchaguzi wa maneno, vilenzi na kadhalika. Ili mradi kuna kila aina ya vitomeo ambavyo vinaweza kuingizwa na kujadiliwa kwa undani katika kuuona muundo kamili wa kazi moja au nyingine ya fasihi. Kwa mfano, hapo awali tumesema kuwa wahusika wapo huru lakini pia nao wanategemeana sana na sehemu zingine. Hao nao, wahusika, hujengwa na vijisehemu vingi vilivyo huru lakini ambavyo navyo hutegemeana, na pia kila kimoja kinategemeana na kukamilishana ili kumfanya mhusika awe kamili na aweze kuhusishwa na wahusika wengine pamoja na vipengele vingine vya riwaya. Tukimwangalia Rehema kwa mfano, katika Nyota ya Rehema, ni wazi kuwa Rehema ni jina huru la kike. Lakini pamoja na mambo mengine hapajina hili limewekwa kwenye uhusiano na nyota (iwe nyota ya mbinguni au nyota ya bahati). Rehema huyo huyo anajengwa na kujitokeza kuwa Rehema maalum wa riwaya hii kwa kutumia maneno huru ambayo nayo yametumiwa kwa makusudi ili kuunda dhamira huru ambazo nazo zimehusiana na mtiririko wa matukio. Matendo na lugha aliyopewa Rehema ni yake tu na hivyo kumtofautisha na Sulubu, Shamim, Adila au wahusika wengine. Lakini hapo hapo, pamoja na sifa zinazomjenga yeye, ametofautishwa na wengine ili kukidhi haja ya vipengele vingine vya riwaya hiyo. Wahusika wengine nao kadhalika, wanaweza kuonekana huru lakini pia humtegemea Rehema na wahusika wengine ili kukamilika na kuifanya riwaya iwe ilivyo.

Kirumbi (1974:6) alijaribu kuangalia muundo wa riwaya na alichagua riwaya ya Ubeberu Utashindwa ili kufanya jaribio hili. Hata hivyo, pamoja na mafanikio kidogo yaliyojitokeza, Kirumbi anakiri kuwa:

Ni muundo unaompa msomaji kazi ya kufikiri na mara nyingine kuiona hadithi ngumu

Pamoja na jitihada hiyo, yeye mwenyewe alishindwa kuutumia uhakiki wa kimuundo na alirudi kulekule kwenye kutumia maelezo na ufafanuzi. Tatizo lililojitokeza, ambalo pia limejitokeza kwa wahakiki wengine kama vile Sengo (1973), Sengo na Kiango (1973), Gibbe (1978 na 1982), Mulokozi (1983), Basha (1977), Ohly (1981) na Mlacha (1984) ni kuwa pamoja na maelezo marefu kuhusu tuseme dhamira au wahusika, wahakiki hao hawakuzichambua mada zao kwa undani hata katika upekee huo. Kwa vile kila kipengele kimeangaliwa juu juu hata uhusiano wake na vipengele vingine haujitokezi kwa kiasi cha kuridhisha. Ohly (1983:30) anapozungumzia juu ya muundo wa kiumbuji anaishia kuangalia maudhui, lugha, na kile anachokiita miundo mingme kama vile ya kiutendaji, kimfanano au ya kusawazisha. Pamoja na kuwa fasili ya Ohly kuhusu muundo ni finyu mno na kile anachokitenga kama muundo si muundo, bali labda mtindo, yeye ameyaangalia rnaudhui kama yaliyojijenga yenyewe bila kutegemeana na sehemu nyingine za riwaya.

Uchambuzi wa riwaya katika kiwango hicho finyu cha dhamira, wahusika na vipengele vingine katika upekee umepitwa na wakati. Ni muhimu hivi sasa kujifunza kuiangaiia riwaya kwa undani zaidi na kwajicho la uhakiki wa kila anachokitumia na kuzungumzia mwandishi, namna anavyokizungumzia na pia kukihusisha na sehemu nyingine zote. Hivyo basi, tuangalie muundo ni nini na kuona ni vipi uchambuzi wa kimuundo una manufaa katika fasihi ya Kiswahili.

Uchambuzi wa kimuundo si maarufu sana katika fasihi ya Kiswahili ingawa imedhihirika (Mlacha: 1987) kuwa ndiyo njia mojawapo maridhawa ya kuweza kuiangalia riwaya ya Kiswahili na kuona namna ilivyojengwa. Muundo wa riwaya ni namna kazi ilivyopangwa na ni mshikamano wa kila kitu kilichotumika katika kuijenga kazi hiyo. Kwa wahakiki wengine, hasa wale wakiumbo hapo zamani, waliona kuwa hilo lilikuwa umbo la kazi ya fasihi na wala sio muundo. Baada ya muda wengi kati yao walikubaliana na wazo kuwa wakati umbo linaonekana baada ya kazi nzima kujengeka, muundo hutumika kuijenga kazi na kutoa umbo. Muundo ukifahamika vyema unaweza kutumiwa kuibomoa kazi na kuijenga tena upya. Hivyo hali ya pekee ya umbo haikamilishi kazi yote na ni sehemu tu ya muundo mzima kama vile sehemu zingine

Nadharia ya muundo ni kati ya njia mojawapo ambayo imepata umaarufu katika uhakiki wa riwaya. Hii ni njia ambayo inaweza kumpa mhakiki nafasi ya kuwa huru kwenye kuiangalia kazi, lakini papo hapo kuelezwa na kazi yenyewe namna ya kuichambua. Muundo, kama nadharia, tunaweza kuuita ni nadharia ya kimapinduzi katika fasihi hasa kwa vile ni njia nyingine tofauti ukilinganisha na mitindo mingme ya zamani. Kwa ujumla kuiangalia riwaya kimuundo ni kuyachunguza mawazo ya mwandishi yalivyojengwa na namna alivyoweza kutumia nyenzo muhimu ya lugha kufanya hivyo. Vile vile ni uwezo wa msomaji kutafsiri na kusaidiana na mwandishi kutayarisha mfumo maalum wa taarifa na hivyo wote kukaribia kuwa kitu kimoja katika kazi hiyo. Ni kwa uhusiano wa aina hii baina ya mwandishi na mhakiki ambapo kazi nzima inaweza kueleweka kwa upana na undani zaidi.

Tukizingatia tuliyojadili hapo awali itaonekana kuwa kazi ya mhakiki wa kimuundo ni kutanzua miachano kutoka kwenye ukawaida wa lugha wa kifasihi unaojitokeza kwenye kiwango kimojawapo cha aya au kazi ya fasihi (tuseme sintaksia, semi, methali) na kukihusisha kiwango hicho na muundowa kiwango kingine kama vile kiwango cha picha aliyoijenga msomaji kutokana na maudhui baada ya kusoma na kuelewa aya au riwaya hiyo. Pamoja na kuviangalia vipengele vyote na kuviweka katika viwango sawa vya uhusiano ni muhimu zaidi kuunda uhusiano baina ya kazi yenyewe na aina mojawapo ya mawazo nje ya kazi hiyo. Mawazo hayo yanakuwa ni tafeiri ya msomaji kulingana na ujuzi wakena jamii inayohusika. Hivyo, tafsih ya kazi lazima ijidhihirishe yenyewe kwa kuingiza kitu kingine nje ya kazi hiyo. Kwa maneno haya tunamaanisha kuwa msomaji anapozingatia yale yaliyoandikwa na yale aliyo na ujuzi nayo lazima awe macho na kile anachokisema yule anayedhaniwa kuwa mwandishi. Njia mojawapo ya kuona jambo hili ni kuangalia jinsi anayedhaniwa kuwa ndiye msimuliaji wa hadithi (au wakati mwingine mwandishi) anavyoimudu lugha na falsafa anayotiririka nayo katika kuandika hadithi yake. Pia ni muhimu kuzingatia mwandishi huyo anavyomwangalia msomaji wake au anavyotaka msomaji wake awe, kwani kwa namna fulani riwaya imeundwa kutokana na mbinu za mwandishi mwenyewe.

Kazi kubwa na ngumu ya mhakiki ni kuwa mdadisi na kuona kwa undani ni vipi mbinu tofauti zilivyotumika katika kuijenga riwaya. Mbinu za uundaji wa riwaya ndizo kiini cha riwaya na hizi hujumuisha lugha, uchaguzi wa maneno, uundaji wa sentensi, utumiaji wa mawazo kimantiki, uundaji wa wahusika, dhamira na kadhalika. Njia mojawapo ya kuziangalia na kuziona mbinu hizi kwa usahihi zaidi ni kuisoma riwaya na kuiunda hadithi upya. Kwa mfano unaweza kuiunda hadithi upya kimchoro. Mchoro huo unaweza kuwa halisi au wa kimawazo; nao unaweza kuangaliwa katika hali ya kutegemeana, sambamba, ya kiukinzano, kwa mgeuzo au katika hali ya usawa. La muhimu kuongelea hapa ni kuwa michoro hiyo inaundwa kulingana na jinsi maudhui ya hadithi yanavyolandana na umbo la hadithi nzima. Kwa mfano, katika riwaya yaRosa Mistika tunaweza kuchora michoro mingi ambayo itahusiana kwa namna tofauti. Tunaweza kuanza na uhusiano wa Rosa na baba yake, Mzee Zakaria. Uhusiano wao unaweza kuwekwa kwenye mchoro wa ukinzano ambapo binti anagombana na baba yake. Papo hapo kuna uhusiano wa Rosa na Charles ambao ni uhusiano wa kufanana (wa wapenzi). Uhusiano wao huu unakuwa katika hali sambamba na ule wa Roza na Zakaria. Hata hivyo mahusiano yote haya mawili yanahusiana kwa vile Rosa ni mtoto wa Zakaria na Zakaria anachukizwa na kitendo cha Charles kutaka kufanya mapenzi na Rosa. Kwa upande mwingine kuna uhusiano wa Rosa na Regina na ule wa Regina na Zakaria. Mahusiano yote haya yanaweza kuangaliwa kimaudhui wakati Roea yupo kijijini na anasoma shule ya msingi. Maudhui haya katika sehemu hii ya riwaya yanahusiana na maudhui yanayofuata baada ya Rosa kufaulu kwenda darasa la tisa. Kwa upande wa muundo wa mahusiano haya, kunaweza kuwa na mabadiliko kutokana na mhakiki atakavyoona lakmi hadithi inabakia pale pale na pia muundo wake. Kwa mfano, uhusiano baina ya Zakaria na Rosa kwa upande fulani ni sawa na ule wa Regina na Rosa. Lakini hapo hapo ni tofauti kabisa. Hivyo kwa watu hawa watatu kuna uhusiano wa kukubaliana na kutofautiana. Rosa ni binti wa Regina na Zakaria, lakini wakati kuna mapenzi baina yake na Regina kuna uadui baina yake na Zakaria. Uhusiano na Regina ni tofauti na uhusiano baina ya Rosa na Charles ingawa kwa wote Rosa ana uhusiano nao wa kirafiki. Kwa Regina ni urafiki wa mama na binti yake wakati kwa Charles ni urafiki wa mapenzi ya mvulana na msichana.

Kutokana na mifano iliyotolewa itaonekana kuwa kinachoweza kuukamilisha muundo wa uhusiano katika sehemu hii ya riwaya ni uchunguzi thabiti wa muundo mzima wa sehemu hii. Ni kutokana na kuangalia uhusiano wao kwa kutumia muundo wa juu ambapo muundo uketo au muundo wa ndani unaweza kuonekana. Muundo huo, kama ilivyokwishaelezwa, unaweza kubadilishwa kwa namna yoyote ile ili mradi uhusiano huo ubakie. Hii ina maana kuwa katika kuichambua sehemu hiyo ya hadithi muundo hukataa maana ya wazi ya hadithi hiyo na badala yake kutafuta namna ya kutenga miundo ambayo si rahisi kuiona kwa uwazi. Miundo hii hutokana na kuivunjavunja sehemu hiyo katika vipande vingine ambavyo navyo vinaweza kuvunjwa zaidi. Kwa mfano tunaweza kukiangalia kipande cha uhusiano baina ya Rosa na Regina. Katika kijipande hiki tunaweza kuangalia kwanza maudhui yake. Hapa hatutapata kitu chochote kipya bali mwanya wa kutafakari muundo na hatari ya kuirudia hadithi. Katika maudhui hayo kuna mawazo ambayo yametokana na maneno yanayohusiana na ambayo mwandishi huyatumia na kuunda sentensi. Maneno hayo hayo yanapounganishwa na kuunda sentensi yanaweza kutoa umbo la mfanano, ukinzani, usawa na kadhalika kwa kutumia sauti, maana, mdundo au hata picha ya mawazo. Hivyo tunaweza kuangalia uhusiano wa maneno na kuona maneno hayo yanatupatia maana gani ya wazi na ya ndani. Katika sentensi yoyote ile maana ya neno moja inatokana kwa kiasi fulani na kuwapo kwake katika sentensi hiyo na uhusiano wake na maneno mengine. Maana ya neno moja pia hutokana na uhusiano wake na kundi fulani la maneno ambayo hayapo kwenye sentensi hiyo lakini yana uhusiano wa aina fulani na hilo neno. Haya yote ni mambo ya kuzingatia wakati wa kuangalia muundo wa maneno au sentensi katika aya au riwaya nzima.

Kwa kawaida muundo hukataa uwazi, yaani hukataa wazo au vitu ambavyo kwa ujumla huonekana vina maana moja au ya moja kwa moja na kuwa maana hiyo kwa kawaida ni wazi tunapoiangalia sote. Hilo ni umbo. Vmbo la nje halielezei jinsi kitu kilivyoundwa. Umbo linaweza kutokana na maudhui wakati muundo ni jinsi maudhui hayo yalivyowekwa. Kile kinachoonekana kuwa ni kweli (kwa mfano katika maudhui) wakati mwingine hakihusiani na ujuzi wetu wa ukweli huo au sio kile ambacho tuna ujuzi nacho. Hivyo si uhusiano tu baina ya kazi na ukweli ndio unaojitokeza katika maudhui. Haya huja baadaye na aghalabu sio muhimu sana katika muundo, ni matokeo ya muundo. Muhimu ni kusogea zaidi na kupata mashiko jinsi akili inavyopata ujuzi wa kuiona kazi hiyo ilivyojengeka. Kama asemavyo Terry Eagleton (1983:109) ni kama vile kumuua mtu ili kuchunguza kwa makini zaidi mzunguko wa damu.

Mpaka hapo tunaweza kuangalia muundo wa riwaya ulivyo. Boulton (1975) alisema kuwa tunapenda hadithi hasa kwa sababu mbili: Kwanza kwa kuwa kwetu tayari kujifurahisha na kujiridhisha na njozi, na pili udadisi na nia yetu ya kujua kwa undani kuhusu ukweli. Ingawa mambo haya yanaelekea kupingana, si rahisi kuyapambanua au kuyatenganisha hasa kwa vile yanahusiana sana na muundo. Sababu ya kwanza inahusiana sana na muundo wa juu na sababu ya pili inahusiana na muundo uketo, yaani wa ndani. Miundo hii miwili kwa pamoja ndiyo inayokamilisha muundo wa riwaya kama vile sababu hizo mbili zinavyokidhi haja yetu ya kuperida kusoma hadithi.

Muundo wa riwaya hujumuisha muundo wajuu na ule wa ndani au muundo uketo. Hii ina maana kuwa mtu anaweza kuisoma hadithi na kupata picha ya kile kinachozungumziwa juu juu kwa kutumia muundo wa juu. Muundo wa juu una sifa kuu zifuatazo: kuna mfuatano wa mizani, wa maneno na sentensi, aya, kurasa, sura na hata aina za maandishi na aina nyingine zote ambazo mara nyingi huhusishwa na wazo la fani. Muundo wa juu ndio uchaguzi wa mwandishi kutoka kwenye njia nyingi tofauti zilizowezekana za kuelezea mawazo aliyoyalenga kwenye muundo wa ndani. Kama itakavyoonekana hapo baadaye, muundo wa ndani ndio unaotawla kile mwandishi anachokisema katika muundo wa juu.

Muundo wa juu unaweza kutambulika kwa kutumia njia tatu wakati wa uchambuzi. Aidha njia hizi ndizo zinazotumiwa zaidi na wasomaji wengi wa riwaya ingawa hawatambui kuwa wanashughulikia muundo wajuu tu. Njia ya kwanza ni ile ya mistari. Hii ni namna ya kusoma na kuliona umbo la riwaya kutokana na mwendo wa sentensi kwa kuzingatia muda na nafasi. Ina maana kuwa katika kusoma kwa namna hii tunazingatia mfululizo wa kauli na sentensi unaoelekea kwenye kumvutia msomaji na kumpa habari zinazofuatana na hata kumpa fursa ya kupata maana ya jumla kwa mpango wa kufuata kisa hadi kisa na kurasa hadi kurasa. Njia nyingine ni ile ya uhusiano wa kimantiki kwa kuangalia njia tofauti za umuhimu baina ya sehemu za mfumo thakiri zenye maana. Hii inatokana na kutoa habari zilizo mpya dhidi ya zile zinazofahamika, kucheleweshwa habari katika hadithi au kutoa maana zilizotolewa au kudhaniwa ziliwasilishwa na sentensi. Njia hii hujitokeza kutokana na kauli zenye mvuto ambapo msomaji anaelekezwa kuwekea makini sehemu kadhaa za maana kuliko nyingine. Njia ya tatu ni ile ya namna mwandishi anavyoyaelezea maudhui yake na jinsi maelezo hayo yanavyomruhusu msomaji kujenga taswira au picha ya mawazo ya mwandishi kuhusu kazi nzima. Kwa mfano, mantiki na sintaksia ya aya na jinsi hoja zilivyoelezwa, vyote huchangia katika kutawala mawazo ya msomaji. Kila sentensi huhitaji sauti ya aina yake ambayo inalingana na muundo na maana ya kile alichokiandika mwandishi. Hivyo msomaji anajikuta akiwa na wazo la kufahamu sauti na mawazo yanayokaribiana na yale ya mwandishi.

Muundo uketo au muundo wa ndani katika riwaya unaangalia uhusiano baina ya vipengele na vijipengele vya lugha, umbo, wahusika na kadhalika ili kuweza kuvichambua na kuvifafanua zaidi. Kile kilichoelezewa kwenye muundo wa juu (au kwa maneno mengine muundo wa nje) kinahusishwa na kile kilichojitokeza katika muundo uketo katika hali ya kukamilishana. Mlacha (1987) aliona kuwa kuchambua riwaya kwa njia ya kimuundo ndiyo njia maridhawa ya kuweza kuielewa riwaya ya Kiswahili hasa kwa vile humo ndimo mna mshikamano wa hadithi nzima na ndiyo njia ya kuuona mfuatano na muoano wa matukio yote. Muundo uketo unaruhusu kufanya marejeo kwenye mawazo fulani nje ya lugha na maudhui na hata kutoa hoja juu ya mawazo hayo. Kwenye muundo uketo ndipo wazo kuu la hadithi linapozingatiwa. Aidha hisia na maono ya mwandishi kuhusu tathmini na utendekaji wa maudhui, kauli zake na maana ya sentensi zake hujitokeza katika muundo huu. Kwa hali hii, uhusiano baina ya mwandishi na msomaji unaweza kujitokeza na kuwa wa karibu zaidi.

Faida ya kuzingatia muundo uketo, pamoja na nyingine zilizojitokeza hapa, ni kuwa muundo huu huwa ni msingi thabiti wa kutambua jinsi maudhui na muktadha wa hadithi vinavyoweza kuficha maana kubwa zaidi ya hadithi. Kwa mfano, tukiangalia aya yenye maneno kama vile cheka, funga, pita, kunywa, iba, pigana, meza, chupa tunaweza kupata picha ya mambo ambayo yanaweza kuwepo na kutokea katika aya hiyo. Hata kama aya hiyo imeelezea hali ya vurugu, ambayo kwa muundo wa nje inaweza kudhaniwa kuwa vurugu katika baa, kutokana na jinsi maneno hayo yalivyotumika katika sentensi na kiasi yalivyorudiwa inawezekana kupata taswira tofauti. Picha kamili ya maneno hayo inaweza kupatikana kwa kuyahusisha haya yote na mawazo mengine yanayotokana na aya zingine katika riwaya hiyo, aya ambazo zinaweza kutokana na maneno mengine kabisa ambayo nayo yamezingatia wazo kuu ambalo linaweza kulinganishwa na kufananishwa na wazo lililopatikana awali. Hii inaonyesha jinsi binadamu anavyoweza kuona vitu, matukio au mabadiliko katika dunia kwa kuhusisha vitu vinavyofanana au vinavyotofautiana na vyote (vinavyofanana na vile vinavyotofautiana), ili kuonyesha kile anachotaka kukieleza au kukiona. Ili kuipatapicha kamili yajinsi muundo uketo unavyosaidia kuimiliki riwaya tutaangalia vipengele vyote muhimu kwa undani zaidi na kisha kuvihusisha.

Tukianza na maudhui tunaweza kusema haya ni kama maana ya jumla ya hadithi. Maana ya hadithi hutokana na sentensi, maneno yaliyotumika, na watu walioyatumia kwa kuzingatia mazingira. Kwa kuisoma hadithi mwanzo mpaka mwisho msomaji anapata ujumbe ambao ndio unaoweza kuwa chanzo cha kuweza kuangalia na kuyachambua mawazo muhimu ndani ya hadithi hiyo. Ingawa tunasema kuwa maudhui ni kama uso wa riwaya au umbo na kuwa ndani yake ndimo tunaweza kuona muundo kamili wa hadithi, ili kuelewa maudhui ya hadithi kwa makini zaidi (hatua ambayo ni muhimu sana katika uchambuzi) jambo kubwa la kufanya ni kuyaangalia maudhui hayo yalivyoundwa. Hii ina maana kuwa ni muhimu kuangalia muundo wa juu uliyyojengwa. Hii ndiyo hatua ambayo inaweza kusaidia zaidi katika kuielezea hadithi upya, na vile vile katika kuilinganisha hadithi hiyo na nyingine. Kwa mfano katika riwaya ya Rosa Mistika tuliyoigusia hapo awali tutaona kuwa hadithi nzima inamwelezea Rosa toka alivyoishi kijijini, alivyokwenda shule ya sekondari na kuanza kubadilika, alivyokuwa mtu tofauti kabisa baada ya kwenda Morogoro na alivyobadilika tena baada ya kufika Mwanza hadi anapokufa.

Ingawa mhusika anajengwa kufokana na sifa tofauti za binadamu tunazozifahamu, katika muundo uketo mhusika hujengwa kutokana na maana za kawaida ambazo mara nyingi hazihusiani tu na ujuzi wetu wa sifa hizi bali huhusiana na mchanganyiko wa sifa hizo na sehemu nyingine zote zinazoiunda riwaya. Ijapokuwa mhusika huyo anatokana na picha aliyonayo mwandishi kuhusu mtu anayetaka kumuunda, picha hiyo imefanyiwa marejeo kutoka kwenye kundi la sifa za kimwili, kitabia, kisaikolojia na hata kikauli kulingana na mazingira na matarajio ya binadamu. Hivyo ni muhimu kumwangalia mhusika huyo katika mapana zaidi akiwa pekee na akiwa na wahusika wengine. Hali hii ya kimshikamano inaweza kuelezea kwa undani zaidi kile anachokifanya kila mhusika na wahusika wote, namna wanavyofanya na kwa nini wanafanya kile wanachokifanya. Matokeo yake ni kuwa mhusika anajitokeza si kwa umbo lake tu (mrefu, mfupi, mnene, mwembamba) au kwa taarifa anazotoa bali kutokana na matendo yake mwenyewe na sifa zote za kibinadamu. Vyote hivi kwa kuhusiana zaidi na matendo ya wengine (yake kwa wengine na wengine kwake) huitawala na kuiongoza hadithi. Ili hali hii ya mhusika ikamilike ni lazima vipengele vingine vya riwaya kama vile dhamira, lugha nk. vitahusika sana.

Todorov (1977) akiwaangalia wahusika kimuundo aliwaona kama jina katika sentensi. Tabia zao aliziona kama vivumishi na matendo yao akayaona kama vitenzi. Kwa kumwona mhusika kama kiungo muhimu katika sentensi (katika riwaya), Todorov ameweza kuonyesha pia kuwa mhusika, ili kuwa kamili kama sentensi inavyokuwa kauli kamili, sharti awe na sifa hizo tatu ambazo zimo katika sentensi. Hivyo, hata kama asemavyo Fowler (1977:89) kuwa mwishowe ni mwandishi ndiye hasa anayetawala matendo, mawazo, sifa na kauli zote za mhusika, vyote hivyo sharti vioanishwe na pia kuambatana na mtiririko mzima wa hadithi. Hivyo kwa maneno mengine, kama asemavyo Todorov, hakuna mhusika isipokuwa kwenye vitendo na hakuna vitendo bila mhusika. Vitendo ndivyo vinavyoelezea mtiririko wa matukio katika riwaya na hivyo jukumu la mhusika mmoja na yale anayoyatenda kuhusiana na wahusika wengine ni muhimu kuchunguzwa kwa undani. Maendeleo na mtiririko wa hadithi hutegemea zaidi mfanano na pia kutofautiana kwa tabia na matendo yao. Ni jumla ya uhusiano huu inayounda muundo uketo wa wahusika katika hadithi. Uwezo wao kufikiri, kuhisi na pia kutambua mawazo na matendo ya wengine ndio huzaa mawasiliano baina yao. Mawasiliano haya, yawe ya kuona, kusikia, kuhisi, kuzungumza au hata kugusana ni muhimu katika muundo wa wahusika na wa riwaya nzima.

Baada ya kuchunguzwa hayo ni muhimu kuangalia ni matendo gani ambayo yamehusishwa zaidi katika kuwajenga wahusika wote hao na ni yapi ambayo ni ya wahusika pekee. Kuwaangalia wahusika kwa namna hii kunaweza kuonyesha nafasi ya mhusika/wahusika katika kujenga dhamira kuu na ndogo kwani mawasiliano yao yataashiria mambo muhimu yanayojitokeza na yanayowatawala wote au baadhi yao. Hapo hapo, kama itakavyoonekana chini tukijadili muundo wa dhamira, ni wazi kuwa dhamira kuu nayo itakuwa inahusiana na kuwatawala wahusika. Hii ni kutokana na uhusiano wa kutegemeana.

Dhamira katika riwaya hutegemea zaidi maudhui na wahusika walivyoundwa. Wakati huo huo maudhui na wahusika havipo huru. Ni vitu ambavyo kwa namna moja au nyingine vimetawaliwa na dhamira ili kukamilika kama tulivyogusiajuu. Lugha pia ni kipengele muhimu ambacho pamoja na kutegemea wahusika walivyoundwa, lengo la dhamira na maudhui yanayotakiwa na mwandishi, lugha hutawala vyote hivyo. Ili kuielewa dhamira kuu au dhamira ndogo ni muhimu kuelewa lugha, maneno, misemo, methali na taswira zilizotumika. Lakini hapa tuongelee zaidi kuhusu muundo wa dhamira.

Culler (1975:224) anasema kuwa ili kuishika dhamira ni muhimu kuielewa hadithi, hivyo kuelewa maudhui ya hadithi. Maendeleo na kukua kwa dhamira kuu hutegemea zaidi dhamira ndogo zilivyojengwa. Hata hivyo, kutokana na mjadala uliotangulia itaonekana kuwa dhamira hujengwa kutokana na maisha ya mhusika mkuu katika uhusiano wake na wahusika wengine. Hivyo dhamira ndogo zinaweza kutokana au kujitokeza kutokana na kila mhusika na katika uhusiano baina ya wahusika. Dhamira ndogo, kama vile kila mhusika, zinapata jukumu la kuunda muambatano na umoja sio tu baina yake (dhamira ndogo) bali pia kati yake na dhamira kuu na pia kati yake na wahusika wote. Hivyo wazo lililofumbatwa katika dhamira moja ndogo litahusiana kwa namna ya kufanana au kupingana na lile la dhamira nyingine na kwa ujumla kuijenga dhamira kuu. Ndiyo kusema kuwa kila dhamira ndogo inaweza kuonekana kama waya mmoja katika wavu, kama sehemu ya mfumo ambao kila muundo sawa wa kila dhamira unaweza kuhudumia kama kizuizi au kiunganisho cha muundo mzima. Kwa maneno mengine, kila dhamira ndogo inaundwa kama dhamira huru ikiwa na maelezo au viashirio kwa dhamira kuu. Katika muungano wake na dhamira ndogo zingine kwa ujumla ndipo kuna kuwa na hali ya muambatano na rnshikamano unaozaa dhamira kuu ambayo inatawala riwaya nzima. Hivyo basi, hata hizo dhamira ndogo sio huru hivyo, bali ni sehemu tu ya kitu kizima chenye sehemu nyingi. Dhamira ndogo huwa zinachangia kuijenga dhamira kuu lakini vilevile hupata maana kutokana na dhamira kuu kwani ni kutokana na hali hiyo ndipo zinaweza kuonekana huru.

Umuhimu wa lugha ni katika kuchambua riwaya na kufanya uhakiki wa kimuundo sio katika utamu, urahisi au ugumu wake. Muundo wa lugha hujumuisha vipengele vingi vya lugha kama vile matumizi ya majina, vitenzi, viambishi na kadhalika. Hivi vinaweza kuangaliwa katika upekee na kisha kuhusishwa na vipengele vingine. Kwa mfano inabidi kuwaangalia Mambosasa na Mamboleo (Gamba la nyoka) kuhusiana na maneno yao wanayoyatumia mara nyingi na kuyaweka katika makundi ya kiuhusiano na kisha kuyahusisha maneno na makundi hayo na taswira zilizojitokeza pamoja na dhamira kuu. Umuhimu wa kuangalia lugha kipekee na kisha katika uhusiano wake na vipengele vingine ni kuwa ndani ya lugha ndimo yanamojitokeza mawazo ya juu na ya uketo ya mwandishi. Kuangalia lugha katika muundo uketo ni kuangalia maana za ndani za maneno au sentensi ambazo zinaweza kujitokeza pamoja na kuwa maana za kawaida zitakuwa zimepewa uzito wake katika kuiangalia lugha katika muundo wa juu.

Kwa kuhitimisha, tutaona kuwa kuangalia riwaya kimuundo tunaweza kuipata picha kamili ya riwaya hiyo. Kwa kufanya hivyo tunaweza kuhakiki riwaya moja kwa makini zaidi na kwa uhakika. Njia hii ya uhakiki pia husaidia sana katika kulinganisha kazi moja na nyingine. Pamoja na ugumu wake unaosababishwa na kuiangalia kazi kwa utulivu zaidi na kufuatilia kila neno na kila kipengele cha liwaya, matokeo yake huwa ya manufaa zaidi kuweza kuishughulikia riwaya katika kila hali, kuziona dosari zilizojitokeza katika kazi hiyo na nini mafanikio, endapo hilo linajitokeza kuwa swali muhimu.

www.masshele.blogspot.com

Share.

About Author

Leave A Reply