Saturday, July 20

MADIWANI URAMBO WAWAOMBA WAZAZI KUCHANGIA CHAKULA CHA WATOTO SHULENI

0


 

Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Adam Malunkwi na Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri hiyo Magreth Nakainga wakibadilishana mawazo wakati wa  kikao
cha Baraza la Madiwani cha kupitia taarifa za utekelezaji wa kila Kata wilayani
Urambo Novemba 9, 2018.

 

Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Magreth Nakainga akitoa ufafanuzi
kwa Madiwani wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa kikipitia
taarifa utekelezaji kwa kila Kata wilayani humo.

 

Mbunge
wa Jimbo la Urambo Magreth Sitta  akichangia taarifa ya utekelezaji wa
kila Kata wilayani Urambo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri
ya Wilaya ya Urambo.

 

Baadhi
ya Madiwani wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa kila Kata wakati wa kikao
cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Urambo.

Mwenyekiti wa Halmashauri
ya Wilaya ya Urambo Adam Malunkwi akifungua kikao cha Baraza la Madiwani cha
kupitia taarifa za utekelezaji wa kila Kata wilayani UramboNovemba 9, 2018.

NA
TIGANYA VINCENT-RS TABORA

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya
Wilaya ya Urambo limekubaliana kuwaelimisha na kuwahamasisha wazazi wa
wanafunzi katika Shule mbalimbali za Msingi kuchangia kwa hiari chakula kwa
ajili kuwajengea mazingira rafiki ya kujifunza na kufanya vizuri katika masomo
na mitihani yao.

Maazimio hayo yalitolewa jana na
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Adam Malunkwi kwa niaba ya wenzake wakati wa
kikao cha Baraza hilo lililokuwa likipitia taarifa za utekelezaji wa Kata
mbalimbali za Wilaya ya Urambo.

Alisema hatua hiyo inalenga kuwafanya
wanafunzi wa shule za Msingi Wilayani Urambo kuwa na usikuvu darsani kwa sababu
ya kupata chakula ambacho kitawawesha kutokuwa na njaa wakati walimu
wanafundisha.

Malunkwi alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri hiyo kuendelea kutoa vibali  kwa wazazi  ambao wako
tayari kuchangia kwa hiari kwa ajili ya maendeleo ya watoto wao ili waweze
kupata uji na chakula cha mchana na kuwaepusha kushinda na njaa na hivyo kuwa
na uelewa hafifu.

Alisema wao wakiwa ni Wawakilishi wa
Wananchi kwa ngazi ya Kata watajitahidi kutumia mikutano yao kuwaelimisha na
kuwahamasisha wazazi kuelewa kuwa chakula kwa watoto kinayo nafasi kubwa ya
kuwafanya wafanye vizuri katika mitihani ya kujipima na ile ya kumaliza elimu
ya Msingi na hivyo kuifanya Wilaya nayo kuongoza.

Malunkwi alisema katika maeneo ambayo
wazazi kwa kauli moja wamekubaliana kutoa chakula kwa ajili ya watoto wao
kupata uji na chakula cha mchana kumekuwepo na mafanikio , matokeo mazuri na
maendeleo mazuri ya taaluma kwao.

“Sisi ni wakulima wazuri wa mahindi,
mpunga, viazi, mihogo na maharage…hakuna sababu ya kushindwa kuwasidia watoto
wetu wapate chakula mashuleni na kuwafanya washinde na njaa na kupunguza
usikivu wakati mwalimu anafundisha darasani…kuanzia sasa Madiwani tumeamua
kutoa elimu kwa watu wetu ili waweze kuchangia chakula mashuleni kwa ajili ya
maendeleo ya elimu ya watoto wetu na wilaya yetu”alisisitiza.

Naye Mbunge wa Jimbo la Urambo Magareth
Sitta alisema ni shele za Msingi 16 kati ya shule za Msingi 77 ndio zinatoa
chakula kwa ajili ya wanafunzi na kuwaomba katika shule zilizobaki 61 kuangalia
uwezekano wa kuwasaidia watoto wao ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
Alisema kuwa kinachotakiwa ni
kuwaelimisha ili waweze kuchangia kwa hiari kwa kuzingatia utaratibu uliwekwa
na Serikali.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Urambo
Angelina Kwingwa aliiagiza Idara ya Elimu kuhakikisha inaongeza juhudi ili
kuziwezesha shule za Msingi na sekondari ziweze kufanya vizuri na hatimaye ziwe
za kwanza kimkoa na kumi bora kitaifa.

Aliwataka wadau wote wakiwemo Madiwani
kushirikiana na Idara ya Elimu katika kuweka mazingira ambayo yatawezesha
kuwatayarisha wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao.

Share.

About Author

Leave A Reply