Friday, August 23

machapisho ya Kiswahili, atoa wito kwa Watanzania

0


Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amezindua machapisho saba ya Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) miongoni mwayo ni kitabu cha Kiswahili kwenye vyombo vya habari.

Amesema machapisho hayo ni kama mfupa kwenye mwili wa binadamu kwa sababu lugha hiyo haiwezi kukua kama hakuna machapisho.

Akizindua machapisho hayo Alhamisi Aprili 18,2019  Profesa Ndalichako amewataka Watanzania kuwekeza katika kusoma vitabu ili kujiongezea maarifa na kupanua lugha ya Kiswahili.

Profesa Ndalichako amesema kwa sababu Kiswahili ni kati ya lugha 10 maarufu duniani lazima kuwe na machapisho yanayoweza kutumiwa katika kujifunzia kiufasaha.

“Kuna ule usemi kwamba ukitaka kuwaficha Watanzania kitu basi ficha kwenye vitabu, kasumba hii tuondokane nayo, niwasihi Watanzania tujikite kusoma vitabu,” amesema Profesa Ndalichako.

Ameitaka Tataki inayofanya kazi chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuandaa pendekezo la kupima umahiri wa Kiswahili ili kukifanya kiendelee kutambuliwa duniani.

Kiongozi hiyo wa wizara ya elimu amesema kati ya vitu vinavyokwamisha taasisi nyingi hata kama zinafanya vizuri kitaaluma ni kutokuwa na machapisho.

Awali, Mkurugenzi wa Tataki Dk Ernesta Mosha amesema machapisho hayo ni njia ya kuendelea kuimarisha na kueneza lugha hiyo duniani.

Dk Mosha ametaja machapisho  mengine kuwa ni Jifunze Kiswahili hazina ya Afrika, Kamusi ya Kiswahili, Lugha na Masuala ibuka na Fasihi ya Kiswahili, Lugha ya Kiswahili na Kamusi ya Kiswahili- Kiitaliano.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere- Taaluma za Kiswahili, Aldin Mutembei amewasisitiza vijana kujifunza Kiswahili na lugha nyingine za kimataifa kutokana na fursa nyingi zilizopo.

“Endeleeni kujifunza lugha nyingine nyingine za kimataifa tena muwe mahiri na niwaambie tu lugha zinazo zungumzwa kwa wingi duniani ni Kichina, kisiponiola na Kiingereza kwa hiyo nyie jifunzeni hizo ili Kiswahili iwe fursa katika kuzitumia,” amesema.

Share.

About Author

Leave A Reply