Friday, August 23

KUNA WAKATI MAPENZI YANAFIKA MWISHO , USILAZIMISHE!

0NIANZE kwa kumshukuru Mungu kwa kunijalia kuiona siku hii ya leo nikiwa mzima wa afya. Ni matumaini yangu kwamba na wewe msomaji wangu uko poa kabisa, karibu kwenye ukurasa huu tubadilishane mawazo na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu uhusiano wa kimapenzi.  Leo nataka kuzungumza na watu ambao wamefikia mwisho wa safari yao ya kimapenzi lakini hawataki kukubaliana na ukweli. Hakuna mtu anayemshauri mtu kuachana na mwenzi wake wala hakuna anayependa kuachana na mwenzi wake waliyeishi pamoja kwa muda mrefu lakini kuna hatua inafika, unakosa njia nyingine zaidi ya kumuacha aende.

Imewahi kukutokea kwamba licha ya kuwahi kumpenda au kupendana na mtu fulani, imefika hatua mambo yote hayawezi kuendelea tena, moyo umekinai, hisia zimekufa na jambo pekee unalotaka litokee ni wewe na mwenzi wako kuachana? Kwamba huamini kama kuna jambo lolote linaloweza kuwafanya mkaendelea kukaa pamoja tena, dunia yenu ya mapenzi imefika mwisho na hakuna tena cha ziada! Mnapofikia hatua hii, wengi huwa wanashindwa kuukubali ukweli, matokeo yake wanasababisha matatizo ambayo yangeweza kuzuilika mapema.

Sishauri watu waachane isipokuwa nachotaka kujadiliana na wewe msomaji wangu ni namna bora inayoweza kutumika kumaliza penzi ambalo haliwezi tena kuendelea. Tunashuhudia kila siku watu wakiachana kwa matatizo makubwa, wakifanyiana ugomvi mkubwa, kupigana, kutukanana, kutoleana kashfa za kila aina, eti kisa mapenzi yamefika mwisho.

Unafikiri ni sawa kuachana kwa vurugu kiasi hicho wakati mliwahi kuishi pamoja kwa amani, upendo na mahaba ya nguvu? Nini huwa kinasababisha baadhi ya watu wanakuwa na tabia za aina hii? Inapotokea umefanya kila kitu kulitetea penzi lako lakini imeshindikana, ni busara kuukubali ukweli kwa sababu mwisho wa mapenzi siyo mwisho wa maisha. Huwezi kujua Mungu anakuepusha na nini, kubaliana na hali halisi kwa sababu inatokea na wewe siyo wa kwanza kuachwa au kukataliwa na umpendaye.

Cha msingi ni kujitahidi kutulia, maumivu yapo tena makali lakini ni vyema kujua namna ya kukabiliana na hali hii ngumu bila kusababisha matatizo zaidi. Mlikutana kwa amani, mkapendana lakini penzi lenu halikupangwa kudumu, kubali matokeo na usonge mbele bila kumfanyia mwenzi wako vurugu. Kingine ambacho kinatajwa kusababisha ugomvi kwa wanandoa au wapenzi walioishi kwa kipindi kirefu wanapoachana, ni mgawanyo wa mali au vitega uchumi vilivyopatikana mkiwa pamoja.

Wanaume ndiyo wanaotajwa zaidi kuwanyanyasa wanawake wanaoachana nao kwa kukataa kabisa kugawana vitu vilivyochumwa pamoja. Hakuna haja ya kukomoana, mpe haki yake ili na yeye huko anakokwenda, akayaanze vizuri maisha yake. Kubalianeni wenyewe nani achukue kitu gani, hakuna haja ya kupelekana mahakamani au kuanza kusumbuana kwa vitu ambavyo mnaweza kuvimaliza kwa kutumia busara. Narudia tena kusema kuachana ni jambo baya linaloumiza lakini kuna muda huwa unafika, mnakosa njia nyingine mbadala zaidi ya kuachana.

Kama mlijaliwa kupata watoto, kubalianeni jinsi ya kuendelea kuwalea watoto bila matatizo. Kubaliana na ukweli na maisha yataendelea, jipe moyo kwamba huenda ukampata mwingine ambaye ni bora kuliko huyo unayeachana naye. Kwa leo niishie hapo tukutane wakati mwingine

Share.

About Author

Leave A Reply