Saturday, August 24

China imezindua ‘Chip’ inayoweza kuongea na ubongo wa binadamu

0


Chip ya “Talker Brain” inaweza kufungua fursa ya kutumika katika  maeneo kama vile matibabu, elimu, maisha ya nyumbani na michezo ya kubahatisha ili kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa katika maeneo hayo. Picha|Mtandao.


  • “Chip” hiyo inaweza kusoma taarifa zinazopatikana katika mishipa midogo ya ubongo.
  • ni hatua ya kuboresha ufanisi wa mawasiliano kati ya binadamu na mashine. 
  • Inaweza kutumika katika maeneo kama vile ya matibabu, elimu, maisha ya nyumbani na michezo ya kubahatisha.

Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza China imezindua ‘chip’ ya kompyuta inayoweza kusoma shughuli zinazofanywa na ubongo wa binadamu, ikiwa ni hatua ya kuboresha ufanisi wa mawasiliano kati ya binadamu na mashine. 

“Chip” ni kipande kidogo kinachofanya muunganiko wa sehemu mbalimbali za Kompyuta ambacho kimeundwa na Saketi mbalimbali ambapo  mara zote kipo kwenye mfumo wa “Silcon”. “Chip” ndiyo imebeba mfumo mzima wa umeme kwenye Kompyuta. 
Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la China (CGTN) Chip hiyo iliyopewa jina la  “Talker Brain,” imetolewa katika mkutano wa tatu wa Upelelezi Ulimwenguni uliofanyika katika mji wa Tianjin hivi karibuni.

Chip hiyo imeundwa kwa pamoja na Chuo Kikuu cha Tianjin  kwa ushirikiano wa shirika la Kielektroniki la China.

“Chip hii ya kompyuta inaweza kutambua habari za mishipa midogo kutoka katika mawimbi ya ubongo yanayotokana na mfumo wa usafirishaji, na kisha kuamua amri,” amenukuliwa  Mkurugenzi wa Uhandisi wa Matibabu na Tafsiri wa Chuo Kikuu cha Tianjin, Ming Dong.

“Itasaidia kuboresha ufanisi wa mawasiliano kati ya ubongo na mashine,” ameongeza Dong. 


Chip ya “Talker Brain” inaweza kufungua fursa ya kutumika katika  maeneo kama vile matibabu, elimu, maisha ya nyumbani na michezo ya kubahatisha ili kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa katika maeneo hayo. 

Kwa muktadha huo, teknolojia hiyo ni akili-mali ya China na wanasayansi wa nchi hiyo wanaendelea kufanya utafiti zaidi ili kuwezesha teknolojia hiyo kusambaa duniani na kuleta matokeo chanya katika maisha ya binadamu.

Share.

About Author

Leave A Reply